SIPRI: Ulimwengu unakabiliwa na ushindani mpya wa nyuklia
16 Juni 2025Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm SIPRIimeonya kwamba mataifa mengi duniani yenye silaha za nyuklia yaliendelea kuboresha silaha zake za nyuklia kwa mwaka uliopita na hivyo kuweka mazingira ya ushindani mpya wa silaha hizo.
Katika ripoti yake iliyotolewa leo SIPRI, imesema mataifa yenye nguvu za nyuklia ikiwa ni pamoja na Marekani na Urusi, ambayo yanachukua karibu asilimia 90 ya hifadhi ya dunia yaliutumia mwaka 2024 "kuboresha silaha zilizopo na kuongeza matoleo mapya".
Taasisi hiyo imebainisha katika ripoti yake kwamba Urusi na Marekani zilikuwa na "mipango mikubwa na endelevu ya kuboresha na kubadilisha vichwa vya nyuklia".
Kwa mujibu wa SIPRI, mivutano ya kimataifa imeshuhudia mataifa tisa yaliyo na silaha za nyuklia - Marekani, Urusi, Uingereza, Ufaransa, China, India, Pakistan, Korea Kaskazini na Israel yakipanga kuongeza hifadhi zake.