SIPRI: Ulaya bado yategemea silaha kutoka Marekani
10 Machi 2025Nchi za Ulaya zilizomo kwenye Jumuiya ya NATO ziliongeza zaidi ya maradufu uagizaji wa silaha katika kipindi cha miaka mitano iliyopita, huku ikinunua zaidi ya asilimia 60 ya silaha kutoka nchini Marekani, hii ikiwa ni kulingana na ripoti ya Taasisi ya Kimataifa ya Utafiti wa Amani ya Stockholm (SIPRI) hii leo.
Matokeo haya ya SIPRI yanakwenda sambamba na tangazo la Umoja wa Ulaya kwamba wanakusudia kuimarisha uwezo wa kiulinzi wa bara hilo ili kukabiliana na mabadiliko ya sera za kigeni za Marekani chini ya Rais Donald Trump.
Ripoti hiyo inaitaja Ukraine kuwa muagizaji mkubwa zaidi wa silaha duniani katika kipindi cha 2020 hadi 2024.
Marekani ilisalia kama muuzaji mkubwa wa silaha duniani, kwa mauzo ya nje yaliyofikia asilimia 43, ikifuatiwa na Ufaransa, iliyouza kwa asilimia 9.6.
Manunuzi ya wanachama wa NATO yaongezeka kwa asilimia 105
Katika kipindi hicho hicho, manunuzi ya silaha yaliyofanywa na nchi wanachama wa NATO barani Ulaya yaliongezeka kwa asilimia 105, ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita, na kulingana na Mkuu wa programu ya Mauzo ya Silaha kwenye taasisi hiyo Mathew George, hii inaashiria maandalizi ya mataifa hayo katika kukabiliana na kitisho cha Urusi lakini pia kutokuwa na uhakika juu ya mwelekeo wa baadaye wa sera ya kigeni ya Marekani.
Kulingana na ripoti hiyo, nchi 35 zilipeleka silaha nchini Ukraine katika kipindi cha kati ya 2020 na 2024, huku Marekani ikipeleka asilimia 45 ya silaha, ikifuatiwa na Ujerumani kwa asilimia 12 na Poland asilimia 11. Urusi bado ni nchi ya tatu kwa mauzo ya silaha, licha ya kupungua kwa asilimia 64 ya mauzo ya nje katika kipindi cha 2020-24 ikilinganishwa na miaka mitano iliyopita.
Uwiano huu kwa mara nyingine unaonyesha wazi changamoto itakayojitokeza ikiwa Rais Donald Trump, ataondoa kabisa msaada wa kijeshi kwa Ukraine.
Ongezeko hili la uagizaji wa silaha kutoka nje limeifanya Ulaya kuwa soko kubwa zaidi la silaha za Marekani kwa mara ya kwanza katika kipindi cha miaka 20.
Mataifa ya Ulaya kwa ujumla yalichangia asilimia 35 ya mauzo ya silaha za Marekani mwaka 2020-24, na kuyatangulia mataifa ya Mashariki ya Kati, ambayo manunuzi yalifikia 33.
Kwa upande wa nchi binafsi, hata hivyo, Saudia Arabia imesalia kuwa mnunuzi mkubwa zaidi wa silaha za Marekani.
Ripoti hiyo aidha imesema wakati uagizaji wa silaha wa mataifa ya Mashariki ya Kati ukipungua kwa aslimia 20 kati ya mwaka 2015-19 na 2020-24, nchi nne kati ya kumi zilizopokea silaha kwa wingi zaidi kati ya mwaka 2020-2024 zilitokea eneo la Ghuba, ambazo ni Qatar, Saudi Arabia, Misri na Kuwait.
Licha ya vita katika Ukanda wa Gaza, vilivyoanza Oktoba 2023, hakukuwa na mabadiliko yoyote ya manunuzi ya silaha yaliyofanywa na Israel kati ya 2015 na 2024. Waisraeli wametumia zaidi silaha walizopewa hapo kabla na Marekani, kulingana na ripoti hiyo ya SIPRI.