Hatma ya mpango wa usitishwaji mapigano Gaza mashakani
14 Februari 2025Baada ya siku kadhaa za sintofahamu kuhusu hatma ya mateka hao watatu wanaotakiwa kuachiwa mwishoni mwa juma hili kwa kubadilishana na wafungwa wa Kipalestina, Hamas inatarajiwa leo kutangaza majina yao.
Israel imetishia hapo jana kuyavunja makubaliano legelege ya kusitisha mapigano huko Gaza, ikisema Hamas inapaswa kuwaachia mateka watatu walio hai mwishoni mwa wiki hii, la sivyo wakabiliane na kuanzishwa tena vita huko Gaza, baada ya Hamas kutishia pia kujiondoa kwenye mkataba huo kwa madai kuwa Israel imekuwa ikiyakiuka.
Hata hivyo, Shirika la Msalaba Mwekundu limeelezea wasiwasi wake kuhusu hali ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa na Hamas huko Gaza huku likielezea hitaji la dharura kwa shirika hilo kuwafikia mateka wanaoshikiliwa.
Shirika hilo ambalo limesaidia katika mchakato huo wa kuachiliwa kwa mateka na wafungwa, limetoa wito mara hii wa kufanyika mabadilishano ya faragha na heshima, kufuatia zoezi lililopita ambapo mateka walilazimishwa kuzungumza.
Kwa kiasi kikubwa makubaliano hayo ya kusitisha mapigano yaliyodumu kwa miezi 15 huko Gaza, yamekuwa mashakani tangu Rais wa Marekani Donald Trump alipopendekeza kuwa nchi yake ingelichukua udhibiti wa Gaza na kuwahamisha Wapalestina milioni 2.4 na kuwapeleka katika mataifa ya Jordan na Misri, kauli iliyoibua ukosoaji mkubwa kote ulimwenguni.
Soma pia: Hamas yasema itawaachia mateka zaidi wa Israel
Vyanzo mbalimbali vimeeleza kuwa Saudia Arabia inaongoza juhudi za haraka za mataifa ya Kiarabu ili kuandaa mpango utakaoamua mustakabali waGaza ili kukabiliana na wazo la Trump. Rasimu ya mpango huo utakaojumuisha ujenzi mpya wa Gaza na kuitenga Hamas, itajadiliwa katika mkutano unaotarajiwa kufanyika mwezi huu huko Riyadh.
Matumaini ya wakazi wa Gaza
Wakazi wa Gaza wana matumaini kuwa makubaliano ya usitishwaji mapigano yataendelea kutekelezwa ili hatimaye kuvimaliza kabisa vita hivyo na kuishi kwa amani kama alivyosema moja wao ambaye hakutajwa jina:
"Jambo la kwanza lililonisukuma kurudi ni kwamba nilitamani kurejea katika makazi yangu. Sote tulitamani kurudi na watoto wetu waone nyumba yetu. Hii ndiyo ilikuwa sababu kuu ya kutaka kurudi nyumbani kwangu. Sio shida. Licha ya vifusi na mabomu, tutaishi katika nyumba zetu, kuzijenga upya na kufanya kazi."
Huku hayo yakiarifiwa, watoto kumi na wanne wa Kipalestina, wengi wao wakiwa wanaugua saratani, wamesafirishwa kuelekea nchini Italia kwa matibabu. Jumla ya watu 45 wakiwemo ndugu wa watoto hao, waliondoka na ndege ya kijeshi ya Italia na kulakiwa katika uwanja wa ndege wa Ciampino mjini Rome jana jioni na Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani.
(Vyanzo: AP, AFP, DPA)