IPC yatangaza baa la njaa katika Ukanda wa Gaza
23 Agosti 2025Hali hiyo pia huenda ikawa mbaya zaidi kama misaada ya kitu haitoruhusiwa kuingia kwa wingi katika ukanda huo ambao ni makazi kwa maelfu ya wapalestina.
Njaa inahofiwa kusambaa katika sehemu za Deir al-Balah na Khan Younis ifikapo mwishoni mwa mwezi ujao. Fatme ambaye ni mkaazi wa Gaza amesema hali huko ni mbaya mno
"Hali ni ya kusikitisha. Hata si kama njaa inayoshuhudiwa nchini Somalia. Sio kama janga lolote katika nchi nyingine, kinachoendelea Gaza ni tofauti."
Tangazo la baa la njaa Gaza, limekuja baada ya miezi kadhaa ya onyo kutoka kwa makundi ya misaada kwamba hatua ya Israel kuzuwia chakula kuingia pamoja na mashambulizi yake ya kijeshi zinasababisha njaa miongoni mwa wapalestina hasa watoto.
Waziri wa maendeleo wa Ujerumani asema msaada zaidi unahitajika Gaza
Hata hiyo Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekanusha ripoti ya IPC akiita ya uwongo.
Hapo jana waziri wa maendeleo wa Ujerumani Reem Alabali Radovan, ametoa wito wa kuwepo kwa misaada zaidi kufikishwa katika Ukanda wa Gaza akisema ripoti ya IPC inayoungwa mkono na Umoja wa Mataifa, inaonesha namna eneo hilo linavyopitia hali ngumu ya kibinaadamu.
Baa hilo la njaa kwa kawaida huwa linatangazwa rasmi wakati vigezo fulani vinapopitishwa ikiwemo, asilimia 20 ya jamii kukabiliwa na upungufu wa chakula, asilimia 30 ya watoto kukumbwa na utapiamlo na angalau watu wazima wawili na watoto wanne kati ya watu 10,000 kupoteza maisha kila siku kutokana na njaa au magonjwa yanayotokana na utapia mlo, matukio ambayo yote yameshashuhudiwa Gaza.