Shirika la Maendeleo la Marekani USAID limefungwa rasmi
4 Julai 2025Uamuzi huu, ulioongozwa na Idara ya Ufanisi wa Serikali chini ya Elon Musk, ni sehemu ya juhudi kubwa za kuvunja mashirika ya serikali ya shirikisho yanayoonekana kuwa na ufanisi mdogo au yanayotumia fedha kupita kiasi.
USAID ilianzishwa mwaka 1961 kupitia Sheria ya Misaada ya Kigeni na kwa agizo la Rais John F. Kennedy. Dhamira yake ilikuwa kushirikiana na nchi zinazoendelea kupambana na umasikini uliokithiri na kuimarisha jamii za kidemokrasia zenye ustahimilivu. Kwa miaka mingi, shirika hili limekuwa miongoni mwa mashirika makubwa zaidi ya misaada duniani, likiratibu maelfu ya miradi ya afya, elimu, kilimo, na misaada ya dharura.
Miongoni mwa mafanikio yake makubwa, USAID ilihusika moja kwa moja katika Mapinduzi ya Kijani kwenye kilimo, yaliyosaidia kuokoa maisha ya zaidi ya watu bilioni moja duniani. Shirika hili pia limesaidia kupunguza vifo vya watoto kwa asilimia 69 tangu mwaka 1990, na kupunguza vifo vya UKIMWI na malaria kwa zaidi ya asilimia 50, kwa mujibu wa ripoti mbalimbali za kimataifa za afya.
Serikali ya Trump inasema USAID inaendeshwa kwa gharama kubwa
Hata hivyo, serikali ya Trump ilianza kulifuta shirika hilo mapema mwaka 2025, ikilalamikia gharama kubwa na manufaa madogo. Kufikia mwezi Machi, Waziri wa Mambo ya Nje Marco Rubio alitangaza kuwa zaidi ya asilimia 80 ya miradi 6,200 ya USAID ingesitishwa, na kwamba takribani miradi 1,000 pekee ingeendelea chini ya usimamizi wa Wizara ya Mambo ya Nje. Msaada wa USAID ulitoa mchango mkubwa katika mapinduzi ya kilimo cha kijani, kinachosifiwa kuokoa maisha ya watu bilioni 1 kote duniani.
Mkurugenzi wa zamani wa shirika hilo Andrew Natsios anasema "Nimewasikia wakuu wa nchi wakiniambia kuwa taasisi muhimu zaidi kwao kutoka Washington siyo Wizara ya Ulinzi wala CIA, bali ni USAID, kwa sababu sisi ni nchi inayoendelea, tupo kwenye mchakato wa maendeleo.”
Rubio alitetea hatua hiyo kwa kusema kuwa "malengo ya maendeleo mara chache hufikiwa,” na kwamba USAID ilichangia uzembe na kuongeza chuki dhidi ya Marekani katika mataifa mengine.
Wizara ya mambo ya nje ya Marekani kuratibu programu za misaada
Tangu sasa, amesema, programu zote zilizobaki za misaada zitakuwa zimeunganishwa moja kwa moja na sera za serikali ya Marekani na kusimamiwa na Wizara ya Mambo ya Nje. Ojok Okello ambaye ni mtaalama wa masuala ya maendeleo barani Afrika amesema "Huu ni wakati kwa mataifa hasa ya Afrika kuzingatia mikakati ya kujenga uwezo wao kushughulikia masuala ya maendeleo hasa mifumo ya hudumu msingi ya elimu, afya na kilimo kuweza kukabiliana na pengo la utegemezi litakalojitokeza baada ya USAID kufunga."
Utafiti mpya uliochapishwa katika jarida la The Lancet umetabiri athari kubwa iwapo hatua hizi hazitafutwa. Watafiti wanaonya kuwa kufungwa kwa USAID kunaweza kusababisha vifo vya zaidi ya watu milioni 14 katika kipindi cha miaka mitano ijayo wakiwemo watoto milioni tano wenye umri wa chini ya miaka mitano hasa katika nchi za kipato cha chini na cha kati.
Kwa kuwa Marekani imekuwa mfadhili mkubwa zaidi wa misaada ya kibinadamu duniani, wataalamu wana hofu kuwa pengo lililoachwa na kufungwa kwa USAID linaweza kuwa na madhara yanayofanana na janga la kimataifa au vita vikubwa. Wakati serikali ya Trump ikisifu hatua hiyo kama ushindi dhidi ya matumizi mabaya ya fedha za umma, wakosoaji wanasema gharama halisi italipwa kwa maisha ya mamilioni ya watu.