Shirika la Kimarekani laanza kusambaza misaada Gaza
27 Mei 2025Kwa mujibu wa vyombo vya habari vya Israel, shirika hilo la Kimarekani liitwalo Wakfu wa Kibinaadamu wa Gaza, GHF, limefunguwa kituo chake cha kwanza cha usambazaji misaada ndani ya Gaza, ambapo mamia ya raia walipokea vifurushi vyenye mahitaji muhimu hapo jana.
Soma zaidi: Ujerumani yaikosoa Israel kwa vita vyake huko Gaza
Hata hivyo, hakuna vyanzo huru vilivyothibitisha kuanza kutolewa kwa msaada huo, huku Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yakitilia shaka uaminifu wa shirika hilo wanalolituhumu kutumiliwa na Israel.
Hapo jana, mkurugenzi wa GHF, Jake Wood, alitangaza kujiuzulu wadhifa wake, akisema haoni jinsi shirika hilo linavyoweza kutekeleza majukumu yake likiheshimu misingi ya kibinaadamu na kimataifa. Umoja wa Mataifa umeonya kuwa hali kwenye Ukanda wa Gaza inaelekea kuwa janga la njaa na mauti.