Washirika wa serikali Burkina Faso wahusishwa mauaji ya raia
15 Machi 2025Human Rights Watch limesema waathiriwa wa shambulio hilo wanadhaniwa kutoka katika kabila la Fulani linalotuhumiwa na mamlaka kwa kuyaunga mkono makundi yenye mfungamano na al Qaeda pamoja na kundi linalojiita dola la Kiislamu.
Shirika hilo la Kutetea Haki za Binadamu limeutaka utawala wa Burkina Faso kuchunguza tukio hilo na kuchukua hatua dhidi ya wahusika.
Soma zaidi: HRW yalituhumu jeshi la Burkina Faso kwa kuua makumi ya raia
Hivi karibuni zilisambaa picha za video katika mitandao ya kijamii zikiwaonesha watu 58 wakiwemo wanawake na watoto wanaoonekana wamekufa au katika hatua za mwisho za maisha yao.
Zinawaonesha pia watu wenye silaha waliovalia sare za wanamgambo ambao wameunda makundi ili kuisaidia serikali ya Burkina Faso kupambana na makundi yenye itikadi kali za Kiislamu. Serikali ya Burkinafaso haikupatikana kwa haraka kuzungumzia suala hilo.