Shinikizo la kuundwa serikali mpya Ufaransa baada ya Bayrou
9 Septemba 2025Miongoni mwa wanasiasa wakubwa waliojitokeza hivi leo kuzungumzia hali inavyoendelea nchini Ufaransa ni aliyekuwa waziri mkuu wa nchi hiyo na kiongozi wa sasa wa kundi la Renaissance bungeni, Gabriel Attal, ambaye alimtaka Rais Emmanuel Macron kumteuwa haraka mpatanishi kuzileta pamoja pande hasimu kabla ya kuundwa kwa serikali mpya.
"Ninasema kwa uwazi kabisa kwamba Rais wa Jamhuri yetu lazima amteuwe mtu mashuhuri kutoka nje ya kundi la wanasiasa, na ambaye hatakuwa waziri mkuu, lakini ambaye atapewa jukumu kuwaleta pamoja viongozi wa vyama vya siasa masaa 24 kwa siku kwa kipindi cha wiki tatu zijazo." Alisema Attal.
Akirejelea mazungumzo yake binafsi na Rais Macron, mwanasiasa huyo alisema kila inapotokea hali kama ya nchi yake ambapo hakuna chama chenye wingi wa kutosha bungeni kuweza kuongoza serikali peke yake, bali vinavyopingana vyenyewe kwa wenyewe, "njia pekee ni kuwa na muafaka wa kitaifa."
'Lazima waziri mkuu apatikane haraka'
Kwa upande wake, waziri wa sasa wa mambo ya ndani wa Ufaransa, Bruno Retailleau, amesema ni lazima Macron apate waziri mkuu mpya haraka iwezekanavyo, ili kukwepa shinikizo la maandamano yanayotarajiwa kuanza siku ya Jumatano (Septemba 10).
"Tunahitaji waziri mkuu haraka sana kwani hapapaswi kuwapo na ombwe la madaraka kabla ya maandamano ya Jumatano ya vuguvugu la mrengo wa kushoto." Alisema Retailleau anayeongoza chama cha mrengo wa kulia cha Republican.
Vuguvugu hilo limeitisha maandamano kwa jina "Tufunge Kila Kitu", ambayo yataanza Jumatano, huku tayari vyama vya wafanyakazi vikiwa vimeitisha migomo itakayoanza tarehe 18 mwezi huu wa Septemba.
Kuangushwa kwa Bayrou
Jioni ya Jumatatu (Septemba 8), wabunge waliiangusha serikali ya Bayrou anayeelemea mrengo wa kati kulia, hatua ambayo sasa inamlazimisha Macron kusaka waziri mkuu wa tano ndani ya kipindi kisichozidi mwaka mmoja.
Wabunge 364 walipiga kura ya kutokuwa na imani na Bayrou dhidi ya 194 waliomuunga mkono, na anatarajiwa kuwasilisha rasmi barua yake ya kujiuzulu hivi leo.
Kura hiyo inachukuliwa kama ulipizaji kisasi dhidi ya uamuzi wa Macron wa kulivunja Bunge mnamo mwezi Juni 2024, na kupelekea uchaguzi mpya aliodhani ungeliuimarisha muungano wake wa kisiasa unaoelemea siasa za mrengo wa kati na zinazopendelea mafungamano zaidi na Ulaya.
Lakini bahati nasibu hiyo ilimgeukia Macron na matokeo yake akapata bunge lililogawika zaidi na lisilo na chama chochote chenye nguvu za kutosha kwa mara ya kwanza katika historia ya karibuni ya Ufaransa.
AFP, Reuters