Sheria mpya ya Israel yazidi kuzuia misaada Gaza
14 Agosti 2025Kwa mujibu wa barua hiyo ya pamoja sheria hiyo imekuwa ikitumika mara kwa mara kukataa maombi ya kupeleka misaada katika Ukanda wa Gaza.
Barua hiyo, iliyotiwa saini na mashirika kama Oxfam na Madaktari Wasio na Mipaka (MSF), imeeleza kuwa maombi angalau 60 ya kugawa misaada huko Gaza yalikataliwa mwezi Julai pekee. Mnamo mwezi Machi, serikali ya Israel iliidhinisha kanuni mpya kwa mashirika ya kigeni yasiyo ya kiserikali yanayofanya kazi na Wapalestina.
Wakati hayo yakijiri, angalau Wapalestina 89 wameuawa katika mashambulizi mbalimbali ya Israel katika Ukanda wa Gaza, watu saba wakiuawa kaskazini-magharibi mwa Gaza katika eneo la usambazaji wa misaada ya kibinadamu.
Katika hatua nyengine Serikali ya Italia ilipokea Wapalestina 114 waliokimbia Gaza wakiwemo watoto 31 wanaohitaji msaada wa matibabu.
Waziri wa Mambo ya Nje wa Italia Antonio Tajani amesema, "Pamoja na hayo, tunatumaini kwamba busara itazingatiwa, na kwamba vita vitamalizika haraka iwezekanavyo. Tumeonyesha upinzani wetu kwa operesheni mpya ya kijeshi ya Israel huko Gaza, na tunaendelea kuhimiza Hamas kuwaachilia, bila kuchelewa zaidi, mateka wote wa Israel walioko mikononi mwao.”
Wizara ya Mambo ya Nje ya Italia, imesema watoto hao wanakabiliwa na majeraha makubwa, ulemavu wa viungo, au magonjwa ya kuzaliwa yanayohitaji matibabu maalum.