Sheria mpya kuzuia jamaa za wakimbizi kuja Ujerumani
25 Mei 2025Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt, atawasilisha kwenye Baraza la Mawaziri sheria ya kuzuia familia kuungana tena ambayo itawaathiri baadhi ya wakimbizi.
Wizara ya Mambo ya Ndani imesema sheria hiyo inaambatana na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa kuunda serikali ya mseto kati ya muungano wa vyama vya Kihafidhina unaoongozwa na Kansela Friedrich Merz na chama cha Social Democrats (SPD).
Bunge lapitisha mpango wa kuwakataa wakimbizi wengi zaidi mipakani Ujerumani
Waziri Dobrindt amesema serikali inaazimia kuziba kwa kiasi kikubwa mianya inayowawezesha watu kuingia nchini Ujerumani kwa urahisi na amesisitiza kuwa hii ni njia nyingine ya kuonyesha kwamba sera ya uhamiaji nchini Ujerumani imebadilika.
Hadi sasa, watu wapatao 1,000 kwa mwezi wamekuwa wanaruhusiwa kuingia nchini Ujerumani kuja kuungana na familia zao.
Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani, ameliambia jarida moja la Ujerumani linaloitwa Bild tabloid, kwamba mipango hiyo haitawezekana tena mara sheria hiyo mpya itakapoanza rasmi.