Sharaa asaini makubaliano na kikosi cha Wakurdi
11 Machi 2025Afisi ya rais wa Syria imetangaza makubaliano na mkuu wa kikosi cha wapiganaji wa Kikurdi cha Syrian Democratic Forces, SDF, kuzijumisha taasisi za utawala wa ndani wa eneo la kaskazini magharibi katika serikali ya kitaifa. Mamlaka za Syria chini ya rais wa mpito Ahmed al-Sharaa zimefanya juhudi kuyavunja makundi yenye silaha na kuwezesha udhibiti wa serikali wa maeneo ya nchi nzima tangu kiongozi wa muda mrefu Bashar al Assad alipoondolewa madarakani Desemba mwaka uliopita baada ya zaidi ya miaka 13 ya vita vya wenyewe kwa wenyewe.
Mkataba huo mpya, unaotarajiwa kutekelezwa kufikia mwisho wa mwaka, umesainiwa kufuatia siku kadhaa za machafuko katikati ya eneo la jamii ya wachache ya Waalawi wa Syria ambalo limesababisha kitisho kikubwa ambacho hakijawahi kushuhudiwa kwa uthabiti wa taifa hilo tangu kuanguka kwa Assad madarakani.
Afisi ya rais ilichapisha taarifa Jumatatu iliyosainiwa na pande zote mbili ikiainisha makubaliano kuhusu kuzijumuisha taasisi za kiraia na kijeshi za eneo la kaskazini mashariki mwa Syria katika utawala wa dola la Syria, vikiwamo vituo vya ukaguzi mpakani, uwanja wa ndege na maeneo ya ardhi yenye mafuta na gesi.
Chombo cha habari cha serikali kimetoa picha ya rais Ahmed al-Sharaa akisalimiana kwa mkono na kiongozi wa SDF Mazloum Abdi kufuatia kutiwa saini makubaliano hayo. Taarifa hiyo ilisema jamii ya Wakurdi ni kipengee muhimu cha dola la Syria, inayohakikisha haki yake ya uraia na haki zote za kikatiba. Pia ilipinga miito ya migawanyiko, chuki na juhudi za kuleta mafarakano kati ya matabaka mbalimbali ya jamii ya Wasyria.
Abdi amesema hivi leo kwamba mkataba huo ni fursa halisi ya kuijenga Syria mpya. Kiongozi huyo wa SDF ameandika katika ukurasa wake kwenye mtandao wa kijamii wa X kwamba wamejitolea kwa dhati kujenga mustakhbali mwema unaohakikisha haki za Wasyria wote na kutimiza matarajio yao ya amani na utu.
Makubaliano yapokelewa vyema na Wakurdi
Makubaliano hayo yamepokelewa kwa furaha na shangwe na Wakurdi. Taha ni mkazi wa eneo la Wakurdi la Qamishli. "Nauona mkataba huu kama hatua nzuri kwa sababu watu wa Syria wameteseka vya kutosha. Kila tabaka katika jamii limechokana na vita. Tunataka amani. Tunataka amani kwa Wakurdi."
Naye Walat Mohammad alisema, "Tuna furaha kupindukia. Ni ushindi mkubwa. Hongera kwa Wakurdi katika maeneo yote manne ya Kurdistan."
Dalil Ali Jabali, ambaye pia ni mkazi wa Qamishli alisema, "Kama Mkurdi na raia wa Syria, nina furaha kwa kanuni za makubaliano na kufika mwisho kwa vita nchini Syria baada ya miaka 14 ya mgogoro. Mungu akipenda, hatua hii inaashiria mwanzo wa uhuru, ingawa wakati wa kusainiwa makubaliano haya si muafaka kutokana na janga wanalokabiliana nalo ndugu zetu upande wa pwani. Naomba wapate haki zao na Syria iishi kwa furaha na usalama kwa Wasyria wote na Wakurdi pia."
Soma pia: Ahmad al-Sharaa atoa wito wa kudumisha amani Syria
SDF limekuwa kama jeshi la utawala wa ndani wa Wakurdi unaodhibiti maeneo makubwa ya kaskazini na mashariki mwa Syria, yakiwemo maeneo yenye utajiri wa mafuta na gesi, ambayo huenda yakadhihirisha kuwa raslimali muhimu kwa mamlaka mpya wakati wanapojizatiti kuijenga upya nchi hiyo.
Makubaliano mapya pia yanazungumzia kuisaidia dola ya Syria katika mapambano yake dhidi ya mabaki ya wafuasi wa Assad na vitisho vyote kwa usalama wa nchi na umoja. Mamlaka mpya za Syria zilitangaza jana mwisho wa operesheni dhidi ya wafuasi wa Assad ambao shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu la Syria lilisema walikuwa wamewaua raia kiasi 1,068, wengi wao wanachama wa jamii ya wachache ya Waalawi ambao walinyongwa na vikosi vya usalama au makundi ambayo ni washirika wao.
Israel yaishambulia Syria
Wakati haya yakiarifiwa chombo cha habari cha serikali ya Syria kimeripoti mashambulizi kadhaa ya kutokea angani yaliyofanywa na Israel katika mkoa wa kusini wa Daraa Jumatatu usiku. Kwa mujibu wa shirika linalofuatilia masuala ya haki za binadamu la Syria, ndege za jeshi la Israel zimefanya mashambulizi 17 jana usiku zikiyalenga maeneo yaliyokuwa zamani yakidhibitiwa na jeshi la Syria, likiwemo jukwaa la ufuatiliaji wa shughuli za kijeshi na virafu.
Jeshi la Isreal limesema leo kwamba ndege zake za kivita zimelishambulia eneo la kusini mwa Syria usiku wa kuamkia leo, zikiilenga mifumo ya ulinzi na maeneo mengine ya kijeshi katika mashambulizi ya hivi karibuni kabisa katika nchi hiyo jirani yake.
Kwa upande mwingine, waziri wa mambo ya nje wa Marekani Marco Rubio amejadili suala la kuendeleza serikali imara na thabiti nchini Syria. Wizara ya mambo ya nje ya Marekani imesema katika taarifa kwamba Rubio alijadili suala hilo na mwanamfalme wa Saudi Arabia, Mohammed bin Salman, pamoja na masuala mengine kuhusu vitisho vya wahouthi nchini Yemen na ujenzi upya wa Ukanda wa Gaza, katika mkutano uliofanyika Saudia.