Shambulizi la kombora la RSF laua watu 14 Darfur
19 Mei 2025Shambulizi la kombora lililofanywa na vikosi vya kundi la wapiganaji wanamgambo wa Rapid Support Forces (RSF) limewaua watu wapatao 14 jana Jumapili katika kambi inayokabiliwa na baa la njaa katika eneo la Darfur magharibi huko Sudan.
Kwa mujibu wa maafisa wa shirika linalotoa huduma za dharura za uokozi, shambulizi hilo liliilenga kambi ya Abu Shouk, mojawapo ya mamia ya kambi kote nchini zinazotoa misaada katika uwanja wa mapambano tangu vita vilipozuka kati ya jeshi la Sudan na kundi la RSF mnamo Aprili 2023.
Zaidi ya watu 30 wauawa katika shambulizi la RSF, Sudan
Shirika hilo limesema soko na maeneo mengine ndani ya kambi hiyo ikiwemo misikiti na makazi ya watu yaliyo karibu na miundombinu ya umma yalilengwa na kwamba wasiwasi kuhusu usalama uliwazuia waokoaji wa kwanza kuhesabu wahanga wote.
Kambi ya Abu Shouk inawahifadhi maelfu ya watu waliokimbia makazi yao kutokana na machafuko kutoka kwa mizozo ya awali huko Darfur na vita vya sasa.
Tangu kupoteza udhibiti wa mji mkuu Khartoum mnamo mwezi Machi, RSF imekoleza mashambulizi yake dhidi ya El-Fasher, mji wa mwisho mkuu wa jimbo huko Darfur ambao bado unadhibitiwa na jeshi la Sudan - na kambi za wakimbizi wa ndani za Zamazam na Abou Shouk.
RSF iliiteka kambi ya wakimbizi wa ndani
Mwezi uliopita RSF waliiteka kambi ya Zamazam kufuatia uvamizi wa umwagaji damu uliowalazimu watu 400,000 kuikimbia kambi hiyo, ambayo iliwahi kuwa makazi ya watu hadi milioni moja waliolazimika kuyakimbia makazi yao.
Mgogoro wa vita nchini Sudan sasa umeingia mwaka wa tatu na umeigawa nchi hiyo ya kaskazini mashariki mwa Afrika, huku jeshi likilidhibiti eneo la kati, mashariki na kaskazini na RSF wao wakidhibiti karibu eneo zima la Darfur na washirika wake wakiyakamata maeneo ya kusini.
Jeshi la RSF wamefanya mashambulizi kote nchini katika siku za hivi karibuni kujaribu kudhibiti maeneo na kuzifunga njia muhimu za usafirishaji wa mahitaji muhimu.
Wapiganaji wa RSF watuhumiwa kuhusika na uhalifu wa kivita Sudan
Shirika linalofuatilia mzozo wa Sudan linalofahamika kama Emergency Lawyers, Mawakili wa Dharura, limeorodhesha vitendo vya kikatili kwa pande zote mbili na siku ya Jumapili lilituhumu jeshi kwa kuwaua raia 18, wakiwemo watoto wanne, katika shambulizi dhidi ya kijiji cha Al-Hamadi katika jimbo la Kordofan Kusini wiki iliyopita.
Shambulzi hilo linalodaiwa kufanywa na jeshi la Sudan na washirika wao waasi lilifuatiwa na uporaji mkubwa wa makazi ya raia na soko, kutiwa ndani kwa wanaharakati na watu kadhaa wakilazimika kukimbia kwa miguu kuelekea miji na vijiji jirani.
Pande zote mbili zimetuhumiwa kwa kufanya uhalifu wa kivita ukiwemo kuwalenga raia, mateso na uporaji au uzuiaji wa misaada ya kibinadamu.