Qatar yalaani "ugaidi wa serikali” ya Israel, Trump 'akerwa'
10 Septemba 2025Qatar imesema shambulizi hilo lilihusisha makombora yaliyopenya bila kutambuliwa na mifumo yake ya ulinzi. Miongoni mwa waliouawa ni mtoto wa kiongozi wa mazungumzo wa Hamas, Khalil al-Hayya, pamoja na walinzi wake kadhaa na askari wa usalama wa Qatar. Doha imelitaja tukio hilo kuwa "ugaidi wa kiserikali” na kudai Israel imekiuka mamlaka yake.
Kwa upande wa Israel, balozi wake katika Umoja wa Mataifa, Danny Danon, alitetea operesheni hiyo akisema haikulenga Qatar bali Hamas. Aliongeza kuwa: "Sio kila mara tunatenda kwa maslahi ya Marekani. Tunashirikiana, wanatupa msaada wa kipekee na tunashukuru, lakini wakati mwingine tunafanya maamuzi kisha tunaiarifu Marekani. Hii haikuwa shambulio dhidi ya Qatar; lilikuwa shambulio dhidi ya Hamas.”
Trump akosoa mshirika wake
Rais wa Marekani Donald Trump alisema hakufurahishwa na shambulio la Israel dhidi ya Qatar, akieleza kuwa hakutaarifiwa mapema. "Sijafurahishwa kabisa na hilo … tumekasirishwa sana na jinsi mambo yalivyotokea. Tunataka mateka warudishwe, lakini hatujafurahishwa na hali nzima,” alisema akiwa na waandishi wa habari mjini Washington.
Trump alisisitiza kuwa uamuzi huo "ulifanywa na Waziri Mkuu Netanyahu” na kuongeza kuwa anaiona Qatar kama mshirika na rafiki mkubwa wa Marekani. Hata hivyo, alibainisha kuondoa Hamas bado ni "lengo la maana.”
Ikulu ya Marekani ilisema Trump hakukubaliana na uamuzi wa Israel na kwamba alikuwa ameuelekeza ujumbe wake Steve Witkoff kuionya Qatar mapema. Lakini Doha ilikanusha hilo, ikisema ilipokea taarifa ya Marekani wakati milipuko ilikuwa tayari inaendelea kusikika mjini Doha.
Mona Yacoubian, mshauri mwandamizi katika Kituo cha Utafiti wa Kimkakati na Kimataifa (CSIS), alisema Trump anaonekana kujihusisha na juhudi za kudhibiti madhara. Kwa maelezo yake, rais huyo "anaelewa wazi na kusikia hasira ambazo Qatar imeonyesha kuhusu shambulizi la Israel. Anafanya jitihada kusisitiza kwamba Marekani haikuidhinisha shambulizi hilo, na pia kupunguza hasira za Qatar ili irejee kwenye jukumu lake muhimu la upatanishi.”
Yacoubian aliongeza kuwa shambulizi hilo litaathiri kwa kiasi kikubwa juhudi za kimataifa kumaliza mzozo wa Gaza na huenda likasababisha mapigano kudumu kwa muda mrefu zaidi.
Ukosoaji wa kimataifa
Shambulizi hilo limekosolewa vikali na mataifa mbalimbali. Urusi ililitaja kama "uvunjaji mkubwa wa sheria za kimataifa” na "shambulio dhidi ya mamlaka na uadilifu wa taifa huru,” likionya linaweza kuongeza mzozo. China pia ilionyesha wasiwasi na kulaani hatua zinazodhoofisha mazungumzo ya usitishaji mapigano Gaza.
Rais wa Uturuki Recep Tayyip Erdogan alisema Israel imegeuka kuwa "taifa la kigaidi” linalotumia nguvu za kijeshi kujitanua. Sheikh Zaidi Al-Nahyan wa Umoja wa Falme za Kiarabu anatarajiwa kuwasili Doha, huku Mwana mfalme wa Saudi Arabia Mohammed bin Salman akitarajiwa kufika kesho kuonyesha mshikamano.
Umoja wa Ulaya kupitia rais wake Ursula von der Leyen umetangaza kusitisha msaada wote wa kifedha kwa Israel na kupendekeza vikwazo vipya dhidi ya mawaziri wenye misimamo mikali na walowezi wa Kiyahudi.
Von der Leyen alisema kile kinachoendelea Gaza ni "jambo lisilokubalika” na kusisitiza kwamba "njaa inayosababishwa na binadamu haiwezi kamwe kutumiwa kama silaha ya vita.”
Lakini waziri wa mambo ya nje wa Israel, Gideon Saar, alijibu akisema Ulaya inatuma "ujumbe mbaya unaowatia nguvu Hamas na mhimili wa misimamo mikali Mashariki ya Kati.”
Vifo na takwimu za vita
Kwa mujibu wa Hamas, watu sita waliuawa kwenye shambulizi Doha, akiwemo mwana wa Khalil al-Hayya, walinzi wake watatu na askari wa usalama wa Qatar. Hata hivyo, viongozi wakuu wa Hamas waliokuwepo kwenye jengo walidaiwa kuokoka.
Kwa jumla, shambulio la Hamas la Oktoba 7, 2023 liliua watu 1,219, wengi wao raia, kwa mujibu wa takwimu za Israel. Mashambulizi ya kulipiza kisasi ya Israel yameua angalau Wapalestina 64,605 wengi wao raia, kwa mujibu wa wizara ya afya ya Gaza inayoongozwa na Hamas, takwimu ambazo Umoja wa Mataifa unazitambua kuwa sahihi.