Shambulizi la Israel lauwa watu watatu Beirut
1 Aprili 2025Lebanon imesema shambulizi la Israel kusini mwa mji wa Beirut limewaua watu wapatao watatu
Jumanne, baada ya Israel kutangaza shambulizi lake la pili la aina hiyo katika kipindi cha miezi minne ya makubaliano ya usitishaji mapigano yanayoyumba kati ya Israel na Hezbollah.
Shambulizi hilo limefanywa bila tahadhari wakati wa sikukuu ya Eid al-Fitr kusherehekea mwisho wa mfungo wa mwezi wa Ramadhani.
Wizara ya afya ya Lebanon imethibitisha kuuwawa kwa watu watatu na imesema wengine saba wamejeruhiwa.
Rais wa Lebanon Joseph Aoun amelilaani shambulizi hilo na kuwatolea wito washirika wa kimataifa wa nchi yake waunge mkono haki yao ya uhuru kamili.
Waziri mkuu wa Lebanon Nawaf Salaam kwa upande wake amesema shambulizi hilo ni ukiukaji wa wazi wa makubaliano ya usitishaji mapigano ambayo kwa kiasi kikubwa yalifikisha mwisho kipindi cha zaidi ya mwaka mmoja wa uhasama kati ya Israel na Hezbollah.