Shambulizi la Israel laua watu 10 katika Ukanda wa Gaza
11 Aprili 2025Wakala wa ulinzi wa umma katika Ukanda wa Gaza umeripoti kwamba shambulizi la alfajiri la kutokea angani lililofanywa na jeshi la Israel leo limewaua watu kumi wa familia moja, wakiwemo watoto saba, katika mji wa kusini wa Khan Yunis.
Msemaji wa wakala huo Mahmud Bassal amethibitisha kuuwawa kwa watu hao akisema maiti zao zimepelekwa katika hospitali kufuatia shambulizi hilo lililoilenga nyumba ya familia ya al-Farra katika eneo la kati la Khan Yunis.
Jeshi la Israel imesema linafuatilia shambulizi hilo. Watu walioshuhudia wameripoti kuhusu mashambulizi makali ya vifaru vya Israel huko Khan Yunis.
Wakala wa ulinzi wa umma pia umeripoti kwamba watu wawili wameuwawa katika shambulizi lingine la Israel lililolinga kundi la raia katika eneo la Al-Atatra katika mji wa kaskazini wa Beit Lahia.
Mapema leo jeshi la Israel limetoa tahadhari ya dharura kuwataka wakazi waondoke katika maeneo kadhaa ya mashariki mwa mji wa Gaza.