Shambulizi la Israel katika kanisa Katoliki Gaza laua watu 2
17 Julai 2025Matangazo
Shambulizi la Israel kwenye kanisa pekee la Katoliki katika Ukanda wa Gaza limewaua watu wawili huku Israel ikisema kwa kawaida huwa haiyalengi maeneo ya kidini na kujutia madhara yoyote kwa raia.
Kiongozi mkuu wa kanisa Katoliki duniani Baba Mtakatifu Leo XIV amesema amehuzunishwa sana na shambulizi hilo, lililofanyika wakati wakala wa ulinzi wa Gaza ukiripoti kwamba mashambulizi ya Israel yamewaua watu wasiopungua 24 katika eneo hilo la Wapalestina.
Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni amesema mashambulizi dhidi ya raia Gaza hayakubaliki huku waziri wake wa mambo ya nje, Antonio Tajani akiliita shambulizi hilo katika kanisa kuwa tukio kubwa la kutia wasiwasi dhidi ya eneo la ibada ya Kikristo.