Shambulizi la droni la Israel laua watu 12 Gaza
4 Juni 2025Msemaji wa wakala wa ulinzi huko Gaza, Mahmud Bassal, amethibitisha vifo vya watu hao 12 wakiwemo watoto kadhaa na wanawake, kufuatia shambulizi la droni mapema asubuhi ya leo. Bassal ameliambia shirika la habari la Ufaransa AFP kwamba watu wengine wanne wameuliwa katika mashambilizi mengine ya kutokea angani.
Jeshi la Israel halijatoa kauli mara moja kujibu ombi la AFP kuitaka itoe maelezo.
Tangu makubaliano ya usitishaji mapigano yaliposambaratika mnamo mwezi Machi, Israel imeimarisha operesheni zake za kulishambulia na kulisambaratisha kundi la Kipalestina la Hamas, ambalo shambulizi lake dhidi ya Israel mnamo Oktoba 7, 2023 lilisababisha vita vya Gaza.
Shambulizi hilo lisilo la kawaida la Hamas ambalo halikutarajiwa lilisababisha vifo vya watu 1,218, wengi wao raia, kwa mujibu wa majumuisho ya shirika la habari la Ufaransa, AFP, kulingana na takwimu rasmi.
Wizara ya afya katika eneo linalosimamiwa na Hama la Gaza inasema watu wapatao 4,240 wameuliwa katika eneo hilo tangu Israel ilipoanza tena operesheni yake Machi 18, na kuongeza idadi ya vifo hadi kufikia 54,510, wengi wao wakiwa ni raia.
Vituo vya misaada kufungwa kwa muda Gaza
Haya yanatokea wakati wakfu wa utoaji misaada Gaza, GHF, unaoungwa mkono na Marekani, ukisema vituo vya misaada vitafungwa kwa muda hivi leo, huku jeshi la Israel likionya kwamba njia zote kuelekea katika vituo vya usambazaji misaada zinachukuliwa na kuzingatiwa kama maeneo ya mapigano.
Wakfu huo unasema vituo hivyo vitafungwa kwa ajili ya kufanyiwa matengenezo, upangaji upya na kazi ya kuboresha ufanisi na vitaanza tena kufanya kazi kesho Alhamisi.
Wakfu wa misaada wa GHF, ambao rasmi ni juhudi za kibinafsi na ufadhili usiofahamika, ulianza shughuli zake wiki moja iliyopita lakini Umoja wa Mataifa na mashirika mengine ya misaada yamekataa kushirikiana nao kutokana na wasiwasi kwamba liliundwa kushughulikia malengo ya kijeshi ya Israel.
GHF: Tunasitisha huduma kwa muda Gaza
Lakini msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Tammy Bruce amesema, "Wakfu wa misaada Gaza ni shirika huru. Halipokei ufadhili wa kifedha kutoka kwa Marekani. Hata hivyo tunaangala bila shaka njia muafaka na nzuri za kupeleka misaada Gaza bila kutoa ishara za kukanganya wala kauli za kuvuruga. Halipati ufadhili kutoka kwa serikali ya Marekani."
Vifo vya leo vimetokea baada ya hapo jana watu 27 waliuwawa kusini mwa Gaza wakati vikosi vya Israel vilipofyetua risasi karibu na kituo kimoja kinachosimamiwa na kuendeshwa na wakfu huo. Israel imesema tukio hilo linachunguzwa. Katika siku za hivi karibuni Israel ililegeza mzingiro wake katika eneo hilo la Wapalestina, lakini Umoja wa Mataifa unasema wakaazi wote wangali katika hatari ya kukabiliwa na baa la njaa.
Baraza la usalama kupigia kura azimio la kusitisha mapigano Gaza
Kufuatia matukio ya jana, baraza la usalama la Umoja wa Mataifa litalipigia kura hivi leo azimio linalotaka usitishaji mapigano na pasiwepo vizuizi vyovyote katika utoaji wa misaada ya kibinadamu Gaza. Hatua hii inatarajiwa kukwama kutokana na kura ya turufu ya Marekani.
Hii ni kura ya kwanza ya baraza la usalama lenye nchi 15 wanachama kuhusu suala hilo tangu Novemba mwaka uliopita, wakati Marekani, mshirika muhimu wa Israel, pia ilipotia munda azimio lililotaka mapigano yafike mwisho.
Azimio jipya linataka usitishaji mapigano mara moja, upelekaji misaada bila masharti na makubaliano ya kudumu ya kusitisha mapigano Gaza, utakaoheshimiwa na pande zote. Linataka pia kuachiwa huru mara moja kwa heshima na bila masharti kwa mateka wote wanaoshikiliwa na kundi la Hamas na makundi mengine.
Likielezea hali ngumu ya janga la kibinadamu katika eneo hilo la Wapalestina, azimio hilo pia linataka vikwazo na vizuizi vyote viondolewe kuhusiana na upelekaji na uingizaji msaada wa kiutu Gaza.
Wanadiplomasia wamedokeza kwamba Marekani inatarajiwa kutumia kura yake ya turufu kulizuia azimio hilo lisipite. Pia wamesema wawakilishi kutoka nchi 10 wanachama wa baraza la usalama, watakaoliwasilisha azimio hilo, walijaribu bila mafanikio kushauriana na upande wa Marekani.