Shambulio la Marekani laathiri mazungumzo ya nyuklia ya Iran
27 Juni 2025Katika mahojiano na televisheni ya taifa ya Iran, Waziri wa Mambo ya Nje Abbas Araghchi hakuifunga kabisa milango ya mazungumzo mapya kuhusu mpango wa nyuklia wa nchi yake, lakini alidokeza kuwa huenda yasifanyike hivi karibuni.
"Hapana, kwa sasa hakuna makubaliano yoyote kuhusu kuanzisha tena mazungumzo na Marekani. Nasema hili waziwazi: hakuna miadi iliyowekwa, hakuna ahadi iliyotolewa, na hata hatujazungumza kuhusu kuanzisha tena mazungumzo hayo", alisema Araghchi.
Araghchi aliongeza kusema kuwa uamuzi wa Marekani kuingilia kijeshi umefanya mambo kuwa magumu zaidi na changamoto zaidi kwa mazungumzo kuhusu mpango wa nyuklia wa Iran.
Katika sala za Ijumaa, maimamu wengi walisisitiza ujumbe wa Kiongozi Mkuu Ayatollah Ali Khamenei kutoka hapo jana kwamba vita hivyo vilikuwa ushindi kwa Iran.
Kiongozi wa kidini Hamzeh Khalili, ambaye pia ni naibu mkuu wa mahakama ya Iran, aliahidi wakati wa ibada ya sala ya Ijumaa mjini Tehran kwamba mahakama zitawashughulikia watu wanaoshukiwa kuwa wapelelezi wa Israel 'kwa njia ya kipekee'.
Msemaji wa jeshi la Israel, Brigedia Jenerali Effie Defrin, aliwaambia waandishi wa habari Ijumaa kwamba katika maeneo fulani walizidi malengo yao ya operesheni, lakini wanapaswa kuendelea kuwa waangalifu. Defrin amesema hawafuati udanganyifu wowote kwa sababu adui hajabadilisha nia zake. Akiimanisha Iran.
Kwa upande wake, Mkurugenzi wa shirika la Umoja wa Mataifa la Atomiki, IAEA, Rafael Grossi ameiambia Radio France Internationale kwamba uharibifu uliosababishwa kwenye kituo cha Fordo, ambacho kilijengwa ndani ya mlima, 'ni mkubwa sana'.
MSF yakashifu mpango wa misaada wa Gaza
Kwa upande mwingine, Iran itafanya kile ilichokiita mazishi ya 'kihistoria' mjini Tehran siku ya Jumamosi kwa ajili ya watu 60 waliouawa katika vita vyake vya siku 12 na Israel, wakiwemo makamanda waandamizi wa kijeshi na wanasayansi wa nyuklia.
Huku hayo yakijiri, wizara ya afya ya Gaza imesema, zaidi ya watu 72 wameuawa katika saa 24 zilizopita kutokana na mashambulizi ya Israel.
Ijumaaa (27.06.2025), shirika la madaktari wasio na mipaka (MSF) limetoa wito kusitishwa kwa juhudi tata za misaada huko Gaza zinazoungwa mkono na Israel na Marekani, likizitaja kuwa 'mauaji yanayojificha kama msaada wa kibinadamu'.
Shirika la MSF limesema kuwa zaidi ya watu 500 wameuawa katika Ukanda wa Gaza katika wiki za hivi karibuni walipokuwa wakitafuta chakula.