Shambulio linaloshukiwa kuwa la kigaidi laua watu 32 Mali
8 Februari 2025Taarifa hiyo imetolewa leo na maafisa wa Mali na kueleza kuwa shambulio hilo lilitokea jana Ijumaa kwenye eneo linalopatikana kati ya miji ya kaskazini ya Gao na Ansongo.
Vyanzo mbalimbali vinaeleza kuwa kundi la kigaidi linalojiita Dola la Kiislamu IS ndio lilihusika na shambulio hilo, lakini kundi hilo bado halijatangaza kuhusika. Mara kadhaa, barabara inayoiunganisha miji ya Gao na Ansongo imekuwa ikikumbwa na mashambulizi ya makundi ya itikadi kali au majambazi wenye silaha.
Mali, nchi masikini ya magharibi mwa Afrika imetumbukia tangu mwaka 2012 katika hali ya ukosefu wa utulivu kutokana na mfululizo wa mapinduzi ya kijeshi na imekuwa ikijitahidi kukabiliana na mzozo wa usalama eneo la kaskazini. Watawala wa kijeshi wamevunja uhusiano na mkoloni wa zamani Ufaransa na kuimarisha mahusiano ya kisiasa na kijeshi na Urusi.