Shambulio la makombora la Urusi lauwa 34 Sumy, Ukraine
14 Aprili 2025Watu 34 wameuawa na 117 kujeruhiwa baada ya makombora mawili ya Urusi kuupiga mji wa Sumy, kaskazini mwa Ukraine, katika shambulio baya zaidi mwaka huu. Rais Volodymyr Zelenskiy amelitaja shambulio hilo kuwa ugaidi dhidi ya raia waliokuwa njiani kwenda kanisani kwa ajili ya Jumapili ya Matawi, na kumwomba Rais wa Marekani Donald Trump kuitembelea Ukraine ili kujionea madhara.
Trump amelielezea shambulio hilo kuwa “jambo la kutisha” akisema alielezwa kuwa "walifanya makosa", bila kufafanua zaidi. Baraza la Usalama wa Kitaifa la Marekani lilisema shambulio hilo linaonesha umuhimu wa juhudi za Trump kumaliza vita hivyo, lakini Ikulu ya White House haikuitaja moja kwa moja Moscow kuwa mshambuliaji.
Soma pia: Trump: Mazungumzo ya kusitisha vita Ukraine kuleta tija
Wakati huo huo, droni ya Urusi ilishambulia mji wa Odesa na kujeruhi watu watano, huku Sumy ikitangaza siku tatu za maombolezo na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu ikiendelea kuchunguza madai ya uhalifu wa kivita.