Mahakama yasitisha mazishi ya rais wa zamani wa Zambia Lungu
25 Juni 2025Mahakama Kuu ya Pretoria kutoa amri ya muda ya kusitisha mazishi hayo. Uamuzi wa jaji ulitolewa wakati tayari shughuli ya mazishi ilikuwa imeanza na kuongeza mvutano unaoendelea kati ya serikali ya Zambia na familia ya Lungu.
Mwanasheria Mkuu wa Zambia, amefafanua kuwa mahakama ilitoa amri hiyo baada ya hoja ya msingi kuwasilishwa na hivyo kutoa nafasi kwa pande husika kuendelea na majadiliano pamoja na kutafakari mipango bora ya mazishi.
Serikali ya Zambia inataka Lungu afanyiwe mazishi ya kitaifa nyumbani, kitu kinachopingwa na familia ya Lungu, hii ikiwa ni kufuatia uadui wa kisiasa uliodumu kwa muda mrefu baina yake na Rais wa sasa wa Zambia Hakainde Hichilema, hali iliyoacha uchungu kwa familia hiyo.
Wanafamilia ya Lungu waliokuwa wamevalia nguo nyeusi kwa ajili ya mazishi, walikwenda hadi mahakamani katika mji mkuu wa utawala wa Afrika Kusini, Pretoria, kwa ajili ya kusikilizwa kwa kesi hiyo ambayo ingeamua kama anaweza kuzikwa. Bado haiko wazi ni lini jaji atatoa uamuzi.
Lungu, ambaye alikuwa kiongozi wa Zambia kati ya 2015 hadi 2021, alifariki dunia kwa ugonjwa ambao haukufichuliwa katika hospitali ya nchini Afrika Kusini mnamo Juni 5 akiwa na umri wa miaka 68.
Zambia yasisitiza Hichilema kuongoza mazishi ya kitaifa
Maziko ya kitaifa nchini Zambia yalifutwa mara mbili kwa sababu ya kutokubaliana juu ya mipango ya mazishi. Familia yake na wanasheria walisema aliacha maagizo maalum kwamba hatataka Hichilema kuhudhuria mazishi yake, wakati serikali ya Zambia ikisema Hichilema alitakiwa kuongoza mazishi ya kiserikali.
Mwanasheria Mkuu wa Zambia Mulilo Kabesha aliwasilisha hati ya kesi hiyo kwenye mahakama hiyo ya Afrika Kusini siku ya Jumanne iliyotaka zuio la haraka la mahakama la mazishi yaliyotarajiwa kufanyika Jumatano (Juni 25, 2025) hii ikiwa ni kwa mujibu wa shirika la utangazaji la taifa la Zambia ZNBC.
Hati za mahakama zinataka rais huyo wa zamani azikwe nchini Zambia kwa heshima kamili za kijeshi, kama ilivyoagizwa kwenye sheria za Zambia na kwa kuzingatia kwa maslahi ya umma, ZNBC iliripoti.
Lungu na Hichilema walivutana kwa muda mrefu kisiasa
Ibada ya mazishi ya Lungu ilitarajiwa kufanyika katika kanisa moja huko Johannesburg, karibu kilomita 60 kutoka Pretoria, na mazishi yake yangefanyika kwa faragha, imesema familia yake.
Lungu alimshinda Hichilema katika uchaguzi wa urais wa 2016, na serikali yake ikamfunga Hichilema kwa miezi minne mwaka 2017 kwa makosa ya uhaini, baada ya msafara wake kukataa kuupisha msafara wa rais Lungu. Kifungo hicho hata hivyo kilikosolewa vikali.
Kwenye uchaguzi wa 2021, Hichilema alimshinda Lungu na mwaka uliopita Lungu aliishtaki serikali ya Hichilema kwa kuwatumia polisi kuzuia misafara yake na kumuweka kwenye kifungo cha nyumbani, madai yaliyokanushwa na serikali.