Serikali ya Ujerumani yatoa toleo jipya la kitabu kwa ajili ya wageni.
3 Februari 2005Toleo la pili la kitabu cha maelezo kwa wageni nchini Ujerumani, kitabu cha kurasa 240 kilicho na picha na michoro mingi ya rangi za kupendeza, kitatolewa bure. Hata hivyo hiki siyo kitabu cha mtu kusoma tangu mwanzo mpaka mwisho; kwani watayarishaji wa kitabu hiki, wametenganisha vizuri mambo mbalimbali kiasi kwamba, mgeni anaweza kutafuta na kusoma kifungu kile tu kinachomhusu. Kitabu hiki kipo katika lugha mbalimbali: Kijerumani, Kiingereza, Kihispania, Kifaransa, Kitaliano, Kipolo na Kirusi.
Nakala 60,000 tu ndiyo zitatolewa. Hii inamaanisha kitabu hiki hakitakuwa cha muda mrefu. Hata hivyo mwakilishi wa serikali ya Ujerumani kwenye masuala ya uhamiaji, Bi. Marieluise Beck, amesema, kuna CD-ROM pia ya kitabu hiki. Licha ya hivyo kitabu hiki kinapatikana pia kwenye mtandao wa Internet kwenye mfumo wa faili la PDF ambalo linaweza kuchapishwa au kusomwa na kila mtu kutoka kwenye mtandao wa Internet.
Bi. Marieluise Beck alisema, kitabu hiki kinatoa maelezo ya kutosha kwa wageni wanaotaka kuhamia Ujerumani.
"Kwa kweli kitabu hiki ni kwa ajili ya kila mtu anayetaka kuishi Ujerumani, ukiacha watalii. Huu ni msaada kwao ili waweze kujumuika kirahisi kwenye maisha ya kila siku hapa nchini."
Alisema Bi. Marieluise Beck.
Kitabu hiki kina maelezo yote ya msingi kuhusu Ujerumani na kinajumuisha pia mabadiliko yaliyofanywa kwenye sheria ya uhamiaji iliyoanza kutumika hapo Januani – 1 mwaka huu.
Wageni wanaweza kujielimisha mambo mbalimbali kuhusu siasa za Ujerumani na maisha ya wananchi kwa ujumla. Wahamiaji wanaweza pia kusoma maelezo ya taratibu za kupata leseni ya kuendesha motokaa, namna ya kutafuta kazi na kadhalika. Kitabu hiki kinatoa ufafanuzi wa ufupisho wa majina mbalimbali, pia utamaduni na tabia za wananchi katika mikoa mbalimbali.
Bi. Marieluise Beck alisema, wageni wanapofika hapa nchini mara nyingi hujikuta kwenye hali ya mvutano na wenyeji hasa katika miji mikubwa. Mivutano hii inaweza kupunguzwa ikiwa wageni na wenyeji watapewa nafasi ya kuelewana zaidi. Kwa mfano kuna mambo yanayofanywa na wageni yanayowaudhi wenyeji bila ya wao kujua.
Kitabu kipya cha serikali kinanuia kutatua hata mambo haya, licha ya kuwa mwongozo kwa wageni wanaotaka kuishi hapa bila bila ya kujisikia upweke ugenini. Hiki ni kitabu cha kwanza kilicho na maelezo mengi namna hii, kutolewa na serikali ya Ujerumani kwa wageni.
Maelezo mengine kwa wageni wanaotaka kuhamia nchini Ujeruani, yanapatikana pia kwenye mtandao wa Internet, www.justlanded.com. Website hii ina maelezo mengi pia na faida nyingine ya kutumia mtandao wa Internet, kwani wageni wanaoweza kuwasiliana kati yao kwenye majukwaa mbalimbali. Kwa kufanya hivi wahamiaji hushauriana namba ya kufanya mambo mbalimbali au namna ya kuepuka matatizo katika maisha ya kila siku.