Serikali ya Ujerumani, upinzani wakabiliana kuhusu uhamiaji
28 Januari 2025Serikali ya Ujerumani na vyama vya upinzani vimekabiliana kuhusu sera zinazokinzana za udhibiti wa mipaka. Kiongozi wa upinzani Friedrich Merz, anayepigiwa upatu kuwa kansela ajaye, amesema ataendeleza mpango wake akitumia msaada wa mrengo wa kulia ikiwa itahitajika.
Merz anataka kuwepo na udhibiti mkali wa mipakani na polisi ipewe nguvu zaidi, ishara kuwa anaweka uhamiaji kuwa kipaumbele kwenye kampeni zake katika jitihada za kupambana na chama cha siasa kali za mrengo wa kulia, AfD, ambacho msimamo wake wa kupinga uhamiaji umeongezwa sauti na shambulizi la kisu lililosababisha kifo. Muomba hifadhi aliyehusika alikamatwa.
Merz wa chama cha Christian Democratic Union - CDU amesema Kansela Olaf Scholz wa chama cha Social Democratic - SPD na washirika wao katika serikali ya muungano, chama cha Kijani wanapaswa kulaumiwa kama watamlazimu kuwategemea wabunge wa AfD kuupitisha mswada wake. Serikali ya walio wachache ya Scholz inaupinga mswada huo kwa kutoa mapendekezo yake. Waziri wa mambo ya ndani Nancy Faeser amesema, baada ya kushauriana na mawaziri wa majimbo, anataka kupitisha sheria ya kutekeleza mfumo wa Pamoja wa Ulaya wa Hifadhi na kuwapa polisi mamlaka zaidi ya kushika doria kwenye mipaka.