Serikali ya Uganda imepata hasara
10 Mei 2005Kampala:
Serikali ya Uganda imepoteza Dollar zisizopungua millioni nane baada ya meli yake ya mizigo isiyokuwa na bima kuzama mwishoni mwa juma lililopita. Meli hiyo imezama baada ya kugongana na meli nyingine katika sehemu ya Uganda ya Ziwa Viktoria. Bima ya meli hiyo, MV Kabarega imemalizika wakati wake na ilikuwa karibu kukatiwa bima mpya wakati ajali ilipotokea Jumapili karibu na Kisiwa cha Kuye, umbali wa maili za majini 50 kutoka Kampala. Mwenyekiti wa Shirika la Reli la Uganda, Paul Etiang, amesema kuwa Kabarega imezama ikiwa na shehena ya Tani 940 baada ya kugongana na MV Kaawa. Meli zote mbili zinamilikiwa na serikali ya Uganda. MV Kaawa imeweza kurudi taratibu hadi katika Bandari ya Bell mjini Kampala. Shirika la Reli la Uganda lina meli tatu za mizigo na zote hazina bima. Sababu ya ajali hiyo bado inachunguzwa.