Serikali ya Ufaransa ukingoni kuporomoka
8 Septemba 2025Bayrou hana nafasi yoyote ya kushinda kwenye kura hiyo aliyoiitisha mwenyewe, na ni hatua ambayo huenda ikaibua suintofahamu ya kisiasa na kukosekana kwa utulivu kwenye taifa hilo la pili kwa ukubwa kiuchumi barani Ulaya.
Waziri mkuu huyo mwenye umri wa miaka 74 aliyeteuliwa na Rais Emmanuel Macron na kuhudumu katika kipindi cha chini ya miezi tisa, anadhani kwamba huenda kura hiyo itawaunganisha wabunge katika Bunge la Kitaifa lililogawanyika pakubwa kufuatia mapendekezo ya kupunguza matumizi ya umma ambayo yeye anasema yanahitajika ili kukabiliana na ongezeko la nakisi na deni la Ufaransa.
Lakini wapinzani kwenye bunge hilo lenye wajumbe 577 wanasema watatumia fursa hiyo kupindua serikali ya walio wachache ya Bayrou inayoegemea siasa za wastani na mrengo mkali na wa kulia. Hali hii pengine itamrejesha tena Rais Macron kwenye panda shuka za kumsaka mwanasiasa mwingine wa kuliziba pengo hilo.
Baada ya Bayrou kutoa hotuba iliyoelezea kwa kina kuhusiana na hatua kali za kubana matumizi kama njia pekee kuelekea maslahi ya kitaifa, wabunge hii watatoa maoni yao kabla ya kupiga kura ya kuiunga mkono ama kuipinga serikali mnamo Jumatatu mchana ama jioni. Lakini pia wanao uwezo wa kujizuia.
Kura muhimu
Bayrou anahitaji kura nyingi ili asalie madarakani. Ikiwa wengi watapiga kura ya 'hapana', katiba ya Ufaransa inaelekeza kwamba Bayrou atalazimika kuwasilisha barua ya kujiuzulu kwa Macron, jambo ambalo litaitumbukiza Ufaransa katika mgogoro mpya.
Rais Macron mwenye umri wa miaka 47 anajikuta kwenye mashaka haya kufuatia uamuzi wake aliodhani ni wa kistaarabu wa kulivunja Bunge la Kitaifa mnamo Juni 2024 na kusababisha uchaguzi wa wabunge ambao kiongozi huyo wa Ufaransa alitarajia ungeimarisha muungano wake unaoiunga mkono Ulaya katika Baraza la Wawakilishi.
Lakini jaribio lake hilo halikufanikiwa hata kidogo na badala yake likatengeneza mpasuko mkubwa zaidi bungeni, huku kukiwa hakuna kambi ya kisiasa yenye ushawishi mkubwa, hii ikiwa ni mara ya kwanza kwa serikali ya Ufaransa.
Mnamo Septemba, 2024, aliyekuwa Waziri Mkuu na mtetezi wa Macron, Gabriel Attal pia aliondoka baada ya kushindwa kwenye kura ya imani, ambayo ilipigwa baada ya Michezo ya Olimpiki ya Paris na alidumu madarakani kwa miezi minane tu.
Rekodi ya kuhudumu kwa muda mfupi zaidi kwenye taifa hilo inashikiliwa na mpatanishi wa zamani kwenye mchakato wa Brexit, mhafidhina Michel Barnier aliyekuwa Waziri Mkuu kwa siku 90 tu. Baada ya kuchaguliwa mwezi Septemba, aliondolewa kwa kura ya kutokuwa na imani mwezi Disemba.
Hali ni tete bungeni
Wabunge wa mrengo wa kulia na kushoto ambao wanasema watapiga kura dhidi ya serikali ya Bayrou wanashikilia zaidi ya viti 320, huku wale wa msimamo wa wastani na washirika wa kihafidhina wakiwa na viti 210. Mizania hii inaashiria wazi kwamba hakutakuwa na uwezekano kwa waziri mkuu huyu wa sasa kuepuka kuenguliwa, ingawa yeye mwenyewe anawalaumu wapinzani wake bungeni kuungana dhidi yake.
Mpango wa Bayrou, unaojumuisha kuondoa likizo mbili za umma umekuwa akipingwa na wapinzani wake wa kisiasa ambao kwa hakika wana fursa nzuri ya kumuangusha.
Ikiwa Bayrou atashindwa, Macron atalazimika kumtafuta mrithi mwingine ambaye hata hivyo atafanya kazi katika mazingira yaleyale hatarishi, yanayoanzia kwenye matatizo makubwa ya kibajeti ambayo pia yalimkabili Bayrou na watangulizi wake.