Ujerumani yasitisha ufadhili wa uokozi baharini
2 Julai 2025"Hatuachi watu wazame baharini. Kituo!", anasema Askofu wa Kievanjelisti Christian Stäblein. Kwa mwenyekiti wa shirika la misaada la Sea-Eye, Gorden Isler, kusitishwa kwa malipo ni "ishara mbaya sana." Naye mwenyekiti wa kundi la wabunge wa chama cha Kijani (Die Grünen), Britta Haßelmann, anakosoa hatua hiyo: "Ni wazi kwamba hatua hii ya serikali ya mseto itazidisha mgogoro wa kibinadamu katika Bahari ya Mediterania na kusababisha mateso kwa binadamu."
Uamuzi wa serikali ya Ujerumani iliyoundwa na vyama vya CDU/CSU na SPD wa kusitisha msaada wa kifedha kwa shughuli za uokoaji baharini za wakimbizi katika Bahari ya Mediterania umeibua mjadala mkubwa nchini humo. Mashirika ya uokoaji baharini kama Sea-Eye, SOS Humanity, SOS Méditerranée, RESQSHIP na Sant'Egidio yalipokea kwa jumla euro milioni mbili kama ruzuku kati ya mwaka 2023 na 2024. Katika robo ya kwanza ya mwaka huu, yalipokea takriban euro 900,000. Wizara ya Mambo ya Nje ya Ujerumani imethibitisha kuwa hakuna ufadhili zaidi unaopangwa.
Mabadiliko ya sera chini ya serikali mpya ya shirikisho
Waziri wa Mambo ya Nje wa Ujerumani, Johann Wadephul, ambaye daima amekuwa na mtazamo wa shaka kuhusu uokoaji wa kiraia baharini, ametetea msimamo wake. Anasisitiza kuwa Ujerumani itaendelea kuwa mwaminifu kwa misingi ya ubinadamu, lakini akaongeza: "Sidhani kama ni jukumu la Wizara ya Mambo ya Nje kutumia fedha kwa ajili ya aina hii ya uokoaji baharini. Hivyo basi, tumebadilisha sera. Lakini sera yangu inalenga kutumia njia za kidiplomasia kudhibiti harakati hizi za wakimbizi."
Anasisitiza kuwa Ujerumani inapaswa kuelekeza nguvu zake kule ambako kuna uhitaji mkubwa zaidi, kama vile Sudan na Sudan Kusini. Msemaji wa wizara hiyo, Christian Wagner, anaongeza: "Hii haimaanishi kuwa shughuli za uokoaji baharini ambazo pia ni wajibu zitasitishwa. Swali lililopo ni kama uokoaji huo unapaswa kufadhiliwa na serikali." Aidha, anasema kuwa kwa sehemu kubwa, kazi ya uokoaji bado inafanywa na walinzi wa pwani wa Italia. Hata hivyo, watu wengi bado wanajaribu kuvuka safari hiyo hatari.
Mamia wafariki mwaka huu tayari katika Bahari ya Mediterania
Hatari ya safari hiyo inaonekana kwenye takwimu za hivi karibuni: Tangu mwanzo wa mwaka huu, Shirika la Kimataifa la Uhamiaji (IOM) limeripoti vifo au watu waliopotea 748. Njia ya Bahari ya Mediterania kuelekea Ulaya kupitia boti za meli zisizo salama inatajwa kuwa njia hatari zaidi ya wakimbizi duniani. Tangu mwaka 2014, zaidi ya watu 32,000 wamekufa au hawajulikani walipo.
Kwa hiyo, Marie Michel anaeleza kuwa uamuzi huu wa Ujerumani ni "ushahidi wa aibu wa kuvunjwa kwa haki za binadamu katika Bahari ya Mediterania ya kati." Akizungumza na Deutsche Welle, Michel anasema: "Hasa tukizingatia kuwa serikali ya sasa ya mseto iliahidi katika mkataba wake wa serikali kulinda misaada ya kibinadamu na kufuata misingi ya ubinadamu. Euro milioni mbili tayari ilikuwa msaada mdogo sana — ilikuwa ni cheche tu ya mshikamano kwa watu walioko kwenye harakati za kukimbia."
Ufadhili wa shughuli za uokoaji watingishwa
Michel ni msemaji wa kisiasa wa shirika la misaada SOS Humanity. Shirika hilo lisilo la kiserikali lenye makao Berlin limekuwa likifanya shughuli za uokoaji baharini kwa meli yao Humanity 1 kwa miaka kumi sasa, na linasema limeokoa zaidi ya watu 38,000.
Kupunguzwa kwa msaada wa kifedha na serikali ya Ujerumani kunaathiri sana bajeti ya shirika hilo. Michel anasema: "Kwa mujibu wa makadirio yetu, fedha hizo zingeweza kugharamia oparesheni mbili za uokoaji kwa meli yetu ya Humanity 1. Sasa, kuna pengo kubwa la michango ya wahisani, lakini tunategemea mshikamano mkubwa kutoka kwa jamii."
Mashirika ya uokoaji yasisitiza kukataliwa na jamii ya kisiasa
Mei 2025, Marie Michel alikuwa pamoja na SOS Humanity kama mfuatiliaji wa haki za binadamu kwenye meli ya Humanity 1. Shirika hilo linasema walifanikiwa kuwaokoa watu 297 katika oparesheni nne za uokoaji na kuwapeleka katika bandari za Italia za La Spezia, Ravenna na Bari. Lakini Michel anaonya kuwa kazi yao imekuwa ngumu zaidi si tu kwa sababu ya kusitishwa kwa ufadhili wa serikali, bali pia kutokana na hali ya kisiasa barani Ulaya.
"Kile tunachoshuhudia tangu mwaka jana ni kuondolewa utu kwa watu wanaotafuta hifadhi kutoka Kusini mwa dunia kupitia Bahari ya Mediterania ya kati. Watu hawa wananyimwa haki zao za msingi, wanaachwa katikati ya bahari, wanaachwa wafe," anasema Michel. "Na hiyo hali ya kuondolewa utu inaelekezwa pia kwa mashirika ya kiraia ya uokoaji baharini yanayotoa misaada ya kibinadamu."