Serikali ya Netanyahu hatarini kusambaratika
15 Julai 2025Mtandao wa habari wa ynet nchini Israel umeripoti hivi leo kwamba chama chenye imani kali ya madhehebu ya Orthodox nchini Israel cha United Torah Judaism, kinachoiwakilisha jamii ya Haredi, hakiridhishwi na muswada wa sheria uliowasilishwa jana Jumatatu kudhibiti utumishi jeshini wa waumini wa imani kali ya madhehebu ya orthodox.
Wabunge wa chama hicho, akiwemo naibu waziri wa usafiri na waziri anayeshughulikia masuala ya Jerusalem, wanatarajiwa kujiuzulu nyadhifa zao serikalini. Gazeti la Times nchini Israel limeripoti kwamba hatua yao hiyo huenda ikahitaji saa 48 kabla kuanza kutekelezwa, kumpa muda Netanyahu atafakari upya mapendekezo yake.
Chama cha United Torah Judaism kina viti saba katika bunge la Israel, Knesset, lenye jumla ya viti 120. Kujiondoa kwake kutoka kwa serikali ya mseto ya Netanyahu kutaiwacha serikali hiyo na viti 61, na hivyo kuifanya iwe na wingi wa kiti kimoja tu bungeni.
Katika hali inayoweza kukoleza matatizo zaidi kwa waziri mkuu, chama kingine cha imani kali za madhehebu ya orthodox - Shas - huenda pia kikaondoka kutoka kwa muungano wa Netanyahu kuhusiana na mipango hiyo ya utumishi jeshini; na hivyo kumlazimisha Netanyahu ima ajiuzulu ama aongoze serikali yenye idadi ndogo ya wabunge katika bunge.
Suala la kuwasajili wanaume wa Kiisraeli wanaofuata sana dini katika jeshi limekuwa suala nyeti la muda mrefu linaloibua mvutano kwa muungano wa Netanyahu. Wayahudi wengi walio na imani kali zaidi wanaona utumishi wa kijeshi kuwa tishio kwa maisha yao ya uchaji wa Mungu, kwa sababu wanawake na wanaume hutumikia pamoja.
Matumaini finyu kuhusu mazungumzo ya Doha
Haya yanajiri wakati mazungunzo ya kujaribu kutafuta makubaliano ya kusitisha vita Gaza yakiingia hatua muhimu kwa wiki ya pili huko Doha, Qatar. Wapatanishi wako mbioni wakijadiliana kujaribu kupungua tofauti zilizopo kati ya Israel na kundi la Hamas katika kuelekea kupatikana kwa makubaliano, huku watu zaidi ya 20 wakiuliwa katika eneo hilo la Wapalestina.
Mazungumzo hayo yasiyo ya ana kwa ana yanaonekana yamekwama baada ya pande zote mbili kulaumiana kwa kukwamisha makubaliano ya kuachiwa huru mateka na usitishaji mapigano kwa siku 60 kufuatia miezi 21 ya mapigano.
Afisa mmoja mwenye ufahamu wa mazungzmo hayo ambaye hakutaka kutambulishwa, amesema kwa sasa yanajikita kuhusu ramani zilizopendekezwa za kupelekwa vikosi vya Israel katika Ukanda wa Gaza. Wapatanishi kutoka Misri, Qatar na Marekani wanaendelea na juhudi zinazoifanya Israel iwasilishe ramani ya kuondoka Gaza iliyofanyiwa marekebisho, ambayo itakubalika.
Chanzo hicho kimesema wapatanishi wanatafuta njia kulainisha tofauti zilizobaki na kuendeleza kasi ya mashauriano. Wajumbe wa Hamas wamemlaumu waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kuwa ni kizingiti kikubwa katika mazungumzo hayo.
Umoja wa Ulaya wataka hali ya kibinadamu Gaza iboreshwe
Wakati huo huo, mwanadipolomasia Mkuu wa Umoja wa Ulaya Kaja Kallas ameitolea wito Israel ifuatilie utekelezaji wa makubaliano yaliyoafikiwa wiki iliyopita kuboresha hali ya kibinadamu katika Ukanda wa Gaza.
"Kuhusu hilo naweza kusema kwamba tulifikia makubaliano na Waisraeli juu ya utoaji wa msaada wa kibinadamu kwa watu wa Gaza. Lakini bila shaka, sio tu makubaliano, lakini ni utekelezaji wa makubaliano. Tunaona baadhi ya dalili nzuri za malori zaidi kuingia, na usambazaji zaidi wa chakula kwa watu wa Gaza ukifanyika. Lakini bila shaka, tunajua kwamba hii haitoshi na tunahitaji kusukuma zaidi ili utekelezaji wa yale tuliyokubaliana ufanyike kuboresha hali Gaza."
Katika mkataba huo, Israel ilikubali kuruhusu malori zaidi ya misaada kuingia Gaza, kufungua vivuko zaidi vya mpakani, kuboresha usambazaji wa mahitaji ya chakula, kuruhusu tena upelekeji wa mafuta na kazi ya kivifanyia matengenezo vituo vya ugavi wa umeme na usambazaji maji.
Kallas amesema kuna hatua chanya za matumaini lakini bila shaka wanataka kuona mengi zaidi ili uboreshaji halisi na wa kweli wa hali ya maisha ya watu walioko Gaza udhihirike.
Kallas aidha alielezea juu ya hali ya kibinadamu huko Gaza kama "janga" akisema ilimradi haijaimarika, basi sote hatujafanya juhudi za kutosha. "Imekuwa ngumu zaidi kutoa misaada ya kibinadamu kwa vile hakuna mkataba wa usitishaji vita kati ya Israel na kundi la wanamgambo wa Palestina la Hamas." Aliongeza.