Serikali ya mseto mbioni kuundwa nchini Ujerumani,Abdu Mtullya
13 Oktoba 2005
Afisa wa ngazi za juu wa chama cha SDP amethibitisha kwamba mwenyekiti wa chama hicho Franz Münterfering atakuwa naibu kansela na waziri wa kazi katika serikali ya mseto chini ya Kansela Angela Merkel. .
Baada ya mazungumzo ya siku kadhaa wajumbe wa vyama vikuu vya siasa vya Ujerumani wamefikia mapatano ya kugawana madaraka katika serikali inayotarajiwa kuongozwa na Kansela Angela Merkel mwanamke wa kwanza kushika wadhifa huo katika historia ya Ujerumani.
Wizara nane zitakuwa chini ya chama cha SDP ikiwa pamoja hiyo ya bwana Franz Münterfering, ya ajira.Wizara nyingine muhimu yaani , ya fedha pia itakuwa chini ya SDP na waziri wake anatarjiwa kuwa bwana Peer Steinbrück anaetambulikana kuwa mtu mwenye nidhamu kali.
Wakati majina ya mawaziri hao yanatajwa , mazungumzo juu ya kukamilisha lengo la kuunda serikali ya mseto yanaendelea. Kama mazungumzo hayo yatafanikiwa bi Angela Merkel atathibitishwa kuwa Kansela.
Chama cha SDP pia kimetaja jina la bwana Frank Walter- Steinmeier anatarajiwa kuchukua nafasi ya Joschka Fischer kama waziri wa mambo ya nje.
Bwana Steinmeier mwenye umri wa miaka 49 amekuwa mkuu wa utumishi katika ofisi ya Kansela Schröder tokea mwaka 1999.Kwa mujibu wa vyombo vya habari chama cha SDP kimeshindwa kumshawishi waziri mkuu wa jimbo la Brandenburg bwana Matthias Ptatzeck kushika wadhifa huo.
Bwana Martin Koopman wa baraza la Ujerumani la masuala ya nchi za nje amesema ni vigumu kujua ni masuala gani bwana Steinmeier atayapa kipa umbele katika siasa yake.
Hatahivyo wadadisi wanaamini kwamba bwana Steinmeier ataweza kudumisha urari wa maslahi ya pande zote mbili za mseto.
Waziri wa fedha mtarajiwa bwana Peer Steinbrück mwenye umri wa miaka 58 aliwahi kuwa mtekelezaji wa sera za mageuzi wakati alipokuwa waziri wa uchumi na wa fedha. Pia aliwahi kuwa waziri mkuu wa jimbo la North- Rhine Westphalia
Majina mengine yaliyotajwa leo na chama cha SDP ni pamoja , na la bi Ulla Schmidt anaetarajiwa kuendelea kuwa waziri wa afya. Na Brigitte Zypries katika wizara ya sheria.
Sigmar Gabriel aliyekuwa waziri mkuu wa jimbo la Lower Saxony anatarajiwa kuwa waziri wa mazingira.Na aliyekuwa meya wa mji maarufu wa Leipzig Wolfgang Tiefensee atakuwa waziri wa uchukuzi.
Katika baraza hilo vyama vya kihafidhina vinavyoongozwa na bi Angela Merkel vitakuwa na mawaziri sita.Lakini hadi sasa ni jina moja tu ambalo limetajwa, la bwana Edmund Stoiber atakaekuwa waziri wa uchumi na tekinolojia. Hadi sasa bwana Stoiber ni waziri mkuu wa jimbo la Bavaria. Majina mengine yanatarajiwa kufahamika jumatatu ijayo.
Kansela Gerhard Schröder wa SDP, anaeendelea na ziara nchini Uturuki ameshatamka wazi kwamba hatakuwamo katika serikali hiyo ya mseto.