M23 imechukua udhibiti wa mji wa Bukavu
17 Februari 2025Waasi hao wamesema wameuteka mji huo wa mashariki wenye wakazi milioni 1.3 na wenye utajiri wa madini, ili kurejesha hali ya utulivu baada ya kutelekezwa na majeshi ya Kongo. Msemaji wa muungano "Congo River Alliance" unaolijumuisha kundi la M23 Lawrence Kanyuka, amesema vikosi vyao vinajitahidi kuwalinda wananchi na mali zao.
Soma pia: Umoja wa Afrika waonya dhidi ya kugawika kwa taifa la Kongo
Baada ya miaka mingi ya mapigano na hatua za hivi karibuni za kuiteka miji kadhaa, waasi hao hawakukabiliana na upinzani mkubwa kutoka kwa vikosi vya Kongo. Serikali mjini Kinshasa imeahidi kuwa itarejesha utulivu huko Bukavu, lakini hakukuwa na askari wa Kongo eneo hilo, huku wengi wao wakionekana kujiunga na maelfu ya raia waliokuwa wakiuhama mji huo.