Kongo yathibitisha uwepo wa jeshi la Rwanda Goma
27 Januari 2025
Msemaji wa serikali ya Kongo Patrick Muyaya amesema vikosi vya DRC vinapambana kuzuia "janga na mauaji" huku akitoa wito kwa wakazi wa Goma kusalia majumbani mwao na kutojihusisha na vitendo vya uharibifu wa mali na uporaji.
Mapema leo, waasi wa M23 wameingia katikati mwa mji huo ambako hali bado ni tete huku maelfu ya wafungwa wakiarifiwa kutoroka katika gereza moja huko Goma.
Jeshi la Kongo lililopo kwenye mlima Goma, limevurumisha makombora kuelekea kwenye ardhi ya Rwanda.
Msemaji wa jeshi la Rwanda Ronald Rwivanga amesema raia watano wa Rwanda wameuawa na wengine 25 wamejeruhiwa vibaya katika mji wa Rubavu huko Gisenyi, eneo linalopakana na Kongo.
Waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean Noel Barrot ameelaani uvamizi wa M23 huko Goma.
"Barani Afrika, katika eneo la Maziwa Makuu, mapigano yanapamba moto. Wakati Goma inajiandaa kutekwa, Ufaransa inadhihirisha mshikamano wake na Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo na kuheshimiwa kwa eneo lake. Ufaransa inalaani vikali mashambulizi yanayoongozwa na M23, inayoungwa mkono na Wanajeshi wa Rwanda. Vikosi, ambavyo vimesababisha vifo vya walinda amani sita huku maelfu ya raia wakiyahama makazi yao. Ni lazima mapigano yasitishwe na mazungumzo yaanzishwe tena." Alisema
Soma pia:Mpaka wa Kongo-Rwanda yafungwa baada ya waasi wa M23 kuiteka Goma
Juhudi za kimataifa na kikanda za kuutafutia suluhu mzozo huo zinaendelea. Jana, Baraza la usalama la Umoja wa Mataifa liliujadili mzozo huo, huku mkutano wa marais wa Jumuiya ya Afrika Mashariki ukitarajiwa kufanyika siku ya Jumatano.