Shughuli za chama cha Kabila zasitishwa na serikali ya DRC
20 Aprili 2025Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, imesema imekisimamisha chama cha kisiasa cha rais wa zamani Joseph Kabila, siku chache baada ya kuvamiwa kwa mali zake na vyombo vya usalama.
Wizara ya mambo ya ndani ilitowa taarifa iliyoonesha tarehe ya siku ya Jumamosi, ikisema uamuzi huo umechukuliwa kufuatia harakati za chuki zinazofanywa na Kabila ambaye aliwahi kuwa rais wa taifa hilo kwa miaka 18 hadi mwaka 2019.
Kabila bado ni kiongozi wa chama cha kisiasa cha Peoples Party for Reconstruction and Democracy PPRD. Taarifa hiyo pia iliweka wazi kwamba shughuli zote za chama hicho zimesimamishwa nchi nzima.
Hadi sasa hakuna tamko lililotolewa na PPRD. Rais wa sasa wa Jamhuri ya Kidemokrasi ya Kongo Felix Tshisekedi amemtuhumu Kabila kwamba anaandaa kile alichosema ni ''Uasi '' na anaunga mkono muungano unaojumuisha kundi la M23 ambalo linaendesha vita dhidi ya vikosi vya serikali katika eneo la Mashariki mwa nchi.
Kabila mwenye umri wa miaka 53, aliondoka nchini Kongo kabla ya uchaguzi wa rais mnamo mwaka 2023 kwa mujibu wa msemaji wa familia yake.
Lakini mwanzoni mwa mwezi Aprili,ziltoka taarifa zilizowasilishwa na timu yake zilizosema kwamba rais huyo wa zamani amesema atarejea katika tarehe ambayo haikutajwa,kwasababu nchi iko katika hali ''mbaya''.
Lakini pia zipo taarifa ambazo hazijathibitishwa zinazoonesha kwamba ataingia Kongo,au amekwishaingia katika mji wa Mashariki wa Goma.
Msemaji wa familia siku ya Alhamisi alisema kwamba vyombo vya usalama viliendesha msako na kuvamia makaazi ya Kabila, shamba lake huko Mashariki mwa Kinshasa na kwenye eneo la familia yake katika mji mkuu.
Taarifa ya wizara ya mambo ya ndani imekishutumu chama cha Kabila kwa kuunyamazia uovu au kushirikiana nao na kuunga mkono uchokozi unaofanywa na Rwanda.Soma pia: Marais wa Rwanda, DRC wafanya mazungumzo ya kustukiza ya amani Qatar
Wataalamu wa Umoja wa Mataifa, serikali ya Kongo mjini Kinshasa na mataifa mengi yenye nguvu wamesema kwamba kundi la M23 linaungwa mkono na Rwanda,ambayo inakanusha tuhuma hizo.
M23 linahusika na machafuko yaliyoongezeka mashariki mwa Kongo wakiidhibiti miji kadhaa ikiwemo miji mikubwa ya eneo hilo,Goma na Bukavu.
Taarifa iliyotolewa na wizara ya mambo ya ndani ya Kinshasa imesema Kabila ameendelea na kile ilichokiita''Tabia yake ile ile'' linapohusika M23 ambalo hajawahi kulilaani.
Wizara hiyo imemkosoa Kabila ikisema amechukuwa uamuzi wa makusudi wa kuamua kuingia nchini kupitia Goma,mji ambao unadhibitiwa na ''Adui''
Soma pia:DRC: Mgawanyiko waukumba muungano wa rais mstaafu KabilaLakini pamoja na hayo, taarifa nyingine iliyotolewa na wizara ya sheria ya nchi hiyo imesema mwendesha mashtaka mkuu ametakiwa kuanza mchakato wa kisheria dhidi ya Kabila kuhusiana na mwelekeo wake wa kujihusisha na M23.