Serikali mpya yaapishwa rasmi Burundi
6 Agosti 2025Waziri mpya wa Ulinzi, Bi Marie Chantal Nijimbere, amekula kiapo mbele ya Rais Ndayishimiye na Bunge, akiwa miongoni mwa mawaziri wanaounda serikali ya Waziri Mkuu Nestor Ntahontuye.
Serikali hiyo mpya ina jumla ya mawaziri 13, wakiwemo wanaume tisa na wanawake wanne. Mawaziri kumi kati yao ni wapya katika majukumu yao, na wengine watatu walishawahi kuhudumu katika serikali iliyopita.
Baadhi ya wizara zimevunjwa au kufanyiwa mabadiliko ambapo nyingine zimekuwa vitengo ndani ya wizara kubwa. Mfano ni Wizara ya Jumuiya ya Afrika Mashariki, ambayo sasa ni kitengo ndani ya Wizara ya Mambo ya Nje. Hali kadhalika, Wizara ya Haki za Binadamu na Usawa wa Kijinsia sasa iko chini ya Wizara ya Sheria kama idara maalum.
Vijana wapewa nafasi ya uongozi serikalini
Wengi wa mawaziri katika serikali hii ni vijana, akiwemo Gabby Bugaga, ambaye ameteuliwa kuwa Waziri wa Habari na Mawasiliano ya Umma. Akizungumza na Idhaa ya Kiswahili ya DW, Gabby aliyewahi kuwa mwanahabari, amesema atatoa kipaumbele kwa kuhakikisha wananchi wanapata habari wanazozihitaji.
Wizara ya Nishati na Madini imekabidhiwa kwa kijana Hassan Kibaya, ambaye ni mpya kabisa katika siasa za kitaifa. Baba yake, Saidi Kibaya, aliwahi kuongoza Wizara ya Elimu na Tafiti za Kitaaluma.
Mabadiliko haya ya serikali yanatokana na matokeo ya uchaguzi uliopita, ambapo baadhi ya mawaziri walichaguliwa kuwa wabunge. Hii ni pamoja na aliyekuwa Waziri Mkuu, Gervais Ndirakobuca, ambaye sasa ni Mkuu wa Baraza la Seneti.
Kwa mujibu wa wachambuzi wa masuala ya kisiasa, serikali hii mpya inapaswa kuelekeza nguvu zake katika kukuza uchumi, ili kufanikisha malengo ya taifa ya kuwa nchi iliyoendelea kidogo ifikapo mwaka 2040, na nchi iliyoendelea kikamilifu ifikapo mwaka 2060.