Serikali mpya ya Iraq kuundwa 2004
15 Novemba 2003WASHINGTON: Kwa kulingana na taarifa ya gazeti la NEW YORK TIMES, Marekani inataka kuukabidhi utawala wa Iraq kwa serikali mpya ya mpito tayari mwezi wa Juni hapo mwakani. Gazeti hilo liliripoti kwamba mtawala wa mambo ya Kiraiya wa Kimarekani nchini Iraq, Paul Bremer aliwaarifu viongozi wa Kiiraq kwamba serikali mjini Washington imekwisha wafikiana na mpango wake huo. Ripoti hiyo inamkariri Mwenye Kiti wa Baraza Tawala la Iraq, Ahmed Chalabi akisema kuwa ufikapo wakati huo wanajeshi wa Kimarekani wataweza tu kuendelea kuweko Iraq ikiwa wataombwa na serikali ya mpito ya Iraq kubakia nchini. Shirika la Utangazaji la Kimarekani, ABC liliarifu kuwa hapo mwanzoni mwa mwaka ujao viongozi wa makabila kutoka mikoa 18 ya Kiiraq watawateua wawakilishi na viongozi wengine wa kisiasa katika Bunge jipya la Taifa. Bunge hilo litakabidhiwa jukumu la kuichagua serikali mpya ya mpito itakayokabidhiwa madaraka yake kutoka mtawala wa Kimarekani.