Serikali ijayo Ujerumani yaweza kufufua uchumi uliodorora?
22 Februari 2025Nguvu ya kiuchumi ya Ujerumani inategemea pakubwa uzalishaji wa viwanda ambao unachangia karibu robo ya Pato la Taifa. Baada ya miaka miwili ya mdororo wa kiuchumi, Shirikisho la Viwanda la Ujerumani (BDI) lilibainisha kuwa pato la uzalishaji limepungua mno kuliko ilivyokuwa miaka mitano iliyopita. Matokeo yake ni kwamba viwango vya uzalishaji na uuzaji nje ya nchi vimepungua maradufu nchini Ujerumani huku kasi ya manunuzi ya ndani yakipungua pia.
Katika ripoti yao ya hivi punde ambayo hutolewa kila mwaka kwa Baraza la Wataalamu wa serikali ya shirikisho ya Ujerumani , wataalam wa uchumi walitahadharisha kuhusu kuporomoka kwa sekta zote za uchumi, huku jambo linalotia mashaka zaidi ikiwa matokeo yanayoonyesha kuwa ni bidhaa chache za Ujerumani ambazo sasa zinauzwa nje ya nchi.
Ili kujaribu kutafutia suluhu tatizo hilo, makampuni ya Ujerumani yamependekeza mambo mbalimbali ikiwa ni pamoja na kupunguza ushuru na gharama za nishati, kutoa misaada ya kifedha kwa miradi ya uwekezaji, kuwepo sheria zinazorahisisha kazi, kusitisha kwa muda michango kwenye mfuko wa hifadhi ya jamii na zaidi ya yote kuondoa urasimu. Hayo ndio mambo ambayo wafanyabiashara wa Ujerumani wanayatarajia kwa serikali ijayo nchini humo.
Soma pia: Mazingira vs. uchumi: Je, Ujerumani inapaswa kuchagua?
Rainer Dulger, rais wa Shirikisho la Vyama vya Waajiri wa Ujerumani (BDA), alisema wakati wa mkutano wao mwishoni mwa mwezi Oktoba mwaka 2024, kwamba uchumi umedorora, ukosefu wa ajira unaongezeka na Ujerumani si kivutio tena kwa wawekezaji na kusisitiza kuwa wafanyakazi wenye elimu na uzoefu wamekuwa nadra. Dulger amesema kuwa kanuni na urasimu vimekuwa mzigo kwa makampuni na kwamba Ujerumani imepoteza hali ya ushindani duniani.
Ujerumani si kinara tena duniani kwa kuuza bidhaa nje ya nchi
Kwa miongo kadhaa, manufaa ya mtindo wa biashara wa Ujerumani yalitokana na uwezo wake wa kununua nje ya nchi malighafi na vifaa kwa bei nzuri, kisha kuyatumia kwa ustadi wa uhandisi wa Ujerumani na nishati ya bei nafuu ili kuzibadilisha na kuwa bidhaa zenye thamani zilizotengenezwa nchini Ujerumani.
Uvamizi wa Urusi nchini Ukraine, mzozo wa nishati, mfumuko wa bei, na mabadiliko yanayopendekeza mfumo wa uchumi unaoheshimu hali ya hewa, vilipelekea bei ya nishati kupanda na kuathiri zaidi makampuni ya Ujerumani yanayotumia viwango vikubwa vya nishati.
Soma pia:Uchaguzi wa Ujerumani: Wagombea wajibizana kuhusu uchumi, Ukraine, na Vance
Baraza la wataalam limeeleza kuwa sekta muhimu za kiuchumi kama vile za utengenezaji au teknolojia za vifaa vya kielektroniki zimeathiriwa sana, huku viwanda vinavyoshughulikia masuala ya kemikali vikistawi kwa kiwango cha chini baada ya matatizo viliyoyapitia mnamo mwaka 2023.
Kwa ujumla makampuni yote ya Ujerumani yanaomba kupunguzwa kwa kiasi kikubwa bei ya nishati na kuondoa urasimu ili kuifanya Ujerumani kuwa na ushindani tena yakisisitiza kuwa uchaguzi ujao wa Ujerumani utakaofanyika mnamo Februari 23 ndiyo utakaoamua "hatma ya nchi hiyo."
(DW)